Monday, August 14, 2023

DAWASA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA MIRADI SABA

Mamlaka ya  Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa miradi  Saba ya kimkakati  ikiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, mradi wa ujenzi wa mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji na mradi wa maji Kwala. 

Hayo yameelezwa na Kaimu Afisa Mkuu was DAWASA Kiula Kingu  Leo Agosti 11,2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo.

 Kingu amesema Miradi  iliyotekelezwa imegharimu shilingi bilioni 425.9 inalenga  kuongeza wingi wa maji yanayozalishwa na DAWASA, kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuimarisha mfumo wa usambazaji maji na kuimarisha huduma katika maeneo ambayo hayana mtandao hasa  ya pembezoni.

Aidha Kingu ameeleza pamoja na kuwekeza nguvu katika utoaji wa huduma za majisafi, DAWASA imejipanga kikamilifu na kuchukua hatua za makusudi za kuboresha usafi wa mazingira kupitia miradi mikubwa na midogo. Hii ni kwa sababu upatikanaji wa maji unapoongezeka unapaswa uambatane na usimamizi madhubuti wa usafi wa mazingira.

Hata hivyo Mradi mwingine ni wa kujenga mfumo wa kukusanya majitaka na maeneo nufaika ambapo katika awamu hii ni Mbezi beach, Kilongamwima, baadhi ya maeneo ya Kawe na Salasala. Utekelezaji wa mradi umeanza na Wakandarasi wanaendelea na shughuli za maandalizi ya ujenzi.

DAWASA pia imekuja na ubunifu wa kujenga mifumo na mitambo midogo midogo ya kuchakata majitaka inayojengwa maeneo ya pembezoni ambapo zaidi ya lita 780,000 za majitaka zitakuwa zikichakatwa kwa siku. Miradi hii itajumuisha ujenzi wa vyoo vya umma 30 ambavyo vitasaidia kuboresha usafi wa mazingira. 

Ameeleza kwamba miradi hii itasaidia wananchi kupata huduma za usafi wa mazingira kwa gharama nafuu karibu pia Wakandarasi  wanaendelea na ujenzi na gharama za miradi  ni jumla ya shilingi bilioni 25.7 na wanufaika wanakadiriwa kufikia milioni 1.8.

Alimalizia kwa kusema Miradi hii ni ya kisasa na  mfumo wake wa uchakataji majitaka itatoa gesi asilia kwa ajili ya kupikia, itatoa mbolea itakayoweza kutumika katika kustawisha bustani za miti na majani pia maji yatakayochakatwa yataweza kutumika kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji, usafishaji wa barabara na mitaro ama kupoozea mitambo.

No comments:

Post a Comment