TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imetoa viti mwendo kwa wanafunzi wawili wenye ulemavu wanaosoma Shule ya Msingi Muungano iliyopo Wilayani Kibaha.
Aidha imetoa viti vitatu vya ofisini kwa ajili ya walimu wa shule hiyo ili kuwaondolea kero ya upungufu wa viti vya walimu kwenye shule hiyo.
Akikabidhi vifaa hivyo wakati wa mahafali ya 6 ya shule hiyo ya darasa la saba mratibu wa idara ya afya na mahitaji maalumu kutoka Taasisi hiyo Wilson Fungameza alisema kuwa wametoa viti mwendo hivyo baada ya kuona changamoto za wanafunzi hao wanazozipata wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani.
Fungameza ambaye ni muuguzi namba moja Tanzania na namba tano duniani alisema kuwa wamewapatia wanafunzi hao ili kiwarahisishia wazazi kwani walikuwa wakiwabeba kuwapeleka shuleni na kuwarudisha.
"Baada ya mwalimu mkuu kutoa ombi kwetu tuliona kuna umuhimu wa kuwasaidia watoto hao na wazazi kwani ilikuwa ni changamoto kubwa kwao hivyo kuwa na mazingira magumu ya kupata elimu,"alisema Fungameza.
Kwa upande wake katibu wa Taasisi hiyo Omary Punzi alisema kuwa jamii inapaswa kusaidia wanafunzi na watu wenye uhitaji ili waweze kufikia malengo yao kwa kuwapatia vifaa saidizi.
Punzi alisema kuwa kwakuwa taasisi yao inasaidia jitihada za serikali kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu ili kuhakisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Faith Tawe alisema kuwa wanaishukuru taasisi hiyo kwa msaada walioutoa kwani utawapungizia mzigo wanafunzi na wazazi hao na pia viti vitasaidia walimu wakiwa ofisini.
Tawe aliomba wadau wengine wajitokeze kuwasaidia wanafunzi wanaotoka mazingira magumu pia shule ambayo nayo ina changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa majengo.
Akisoma risala ya wahitimu wa shule hiyo Johnson Ernest alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati ambapo yaliyopo ni 188 kati ya madawati 588 yanayotakiwa.
Ernest alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo wanafunzi wengi wanakaa chini ambapo shule hiyo ina wanafunzi 1,175 na ilianzishwa mwaka 2021 na ina walimu 22.
No comments:
Post a Comment