Wednesday, August 23, 2023

KPC WAJADILI MAREKEBISHO YA BAADHI YA SHERIA

KITUO cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) kimefurahishwa na marekebisho ya baadhi ya sheria yaliyofanyika kati ya mwaka 2019-2023 ikiwemo ya uendeshaji wa mirathi ambapo imeongeza adhabu kwa msimamizi wa mirathi anaposhindwa kutimiza wajibu wake kutoka shilingi 2,000 hadi milioni 2.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa kituo hicho Catherine Mlenga mara baada ya kufanya kikao kupitia marekebisho hayo yaliyofanyika kupitia bunge kwa mujibu wa sheria.

Mlenga alisema kuwa kwa mujibu wa sheria kifungu cha 107 (3) cha sheria ya usimamizi wa mirathi sura 352 ni kuwa msimamizi wa mirathi endapo atashindwa kupeleka taarifa za ukusanywaji na ugawaji wa mali ndani ya muda uliopangwa anaweza kuondolewa na kushtakiwa.

"Kabla ya mabadiliko adhabu ilikuwa ni kulipa shilingi 2,000 au kifungo cha miezi sita ambapo sheria hiyo imefanyiwa marekebisho ambapo faini isiyopungua milioni mbili au kifungo kisichopungua miaka miwili,"alisema Mlenga.

No comments:

Post a Comment