Thursday, August 24, 2023

WAENEZI WATAKIWA KUSEMEA MIRADI UTEKELEZAJI ILANI YA CCM

WAENEZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya za Mkoa wa Pwani wametakiwa kuisemea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama.

Hayo yalisemwa Wilayani Bagamoyo na Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Pwani David Mramba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa semina elekezi kwa waenezi wa wilaya za mkoa huo.

Mramba alisema kuwa semina hiyo ililenga waenezi hao kujua majukumu yao kwa wanachama na kwa wananchi ambapo wanapaswa kuielezea miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa kupitia ilani ya chama ya miaka mitano.

"Waenezi wanapaswa kusemea shughuli mbalimbali za chama pamoja na utekelezaji wa ilani kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ambayo inaongozwa na CCM,"alisema Mramba.

Alisema kuwa kuelezea miradi inayotekelezwa kwanza ni kumsaidia Rais Dk Samia Suluhu Hassan kumsemea jitihada anazozifanya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

"Mambo mengi yanafanywa na serikali ya awamu ya sita lakini baadhi hayasemwi lakini mafunzo haya yawe sehemu ya kukitangaza chama na uzuri wa sera zake ili kuwavutia watu kujiunga nacho,"alisema Mramba.

Aidha alisema kuwa waenezi hao kupitia mafunzo hayo kubadilika na kwenda kisasa na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani nyakati za sasa zimebadilika lazima wajitume.

Kwa upande wake Mwenezi wa Kibaha Mjini Clemence Kagaruki alisema kuwa mafunzo jayo watayashusha ngazi ya kata na matawi ili kuboresha utendaji kazi.

Kagaruki alisema kuwa pia yamewajengea uwezo wa kujiandaa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika mwakani na uchaguzi mkuu wa 2025.

Naye Mwenezi wa Wilaya ya Kibiti Juakali Kuanya alisema kuwa atakuwa kiungo muhimu katika kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi na umma kwa ujumla.

Kuanya alisema kuwa atatumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko ambayo yataleta maendeleo kwa wananchi kupitia sera za chama na mipango mbalimbali ya kiwilaya na kitaifa.

Moja ya wakufunzi wa mafunzo hayo Khadija Juma alisema somo alilofundisha ni kuhusu uzalendo ambalo ni muhimu kwa kila Mtanzania kulijua ili kuitetea nchi yake.

Juma alisema kuwa ili watu waweze kutekeleza majukumu yao lazima wawe wazalendo kama ilivyokuwa kwa waasisi wa nchi ambao walitanguliza uzalendo kwanza.

No comments:

Post a Comment