Saturday, August 19, 2023

MNEC HAMOUD JUMAA ATAKA SUALA LA BANDARI RAIS ASISEMWE VIBAYA





MJUMBE wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) Hamoud Jumaa amevitaka baadhi ya vyama vya upinzani nchi kuacha kumsema vibaya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la mkataba wa Bandari badala yake watoe ushauri.

Jumaa aliyasema hayo Kata ya Mtambani Mlandizi Kibaha alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa operesheni ya kuanza maandalizi ya uchaguzi ngazi ya serikali za vijini yenye kauli mbiu ya Simika Bendera.

Alisema kuwa anawashangaa wapinzani kutoa maneno mabaya kwa Rais kuhusu mkataba wa Bandari ambapo walipaswa kutoa ushauri na si kumsema vibaya.

"Suala la mkataba wa bandari ni jambo la msingi na Rais yuko makini na mkataba huo ili kuongeza mapato ya nchi na kama wao wanaona kuna jambo basi washauri na siyo kutoa maneno yasiyofaa,"alisema Jumaa.

Aidha alisema kuwa wanamshukuru Rais kwani ameonyesha uvumilivu mkubwa licha ya kusakamwa kuhusu suala la bandari ambalo mchakato wake bado unaendelea.

"Tumechoka kusikia Rais anasemwa vibaya yule ni kiongozi hivyo lazima aheshimiwe ila tunampongeza kwa ustaamilivu anaouonyesha kwani hawajibu licha ya kusemwa vibaya,"alisema Jumaa.

Aliwataka viongozi kuwajali viongozi wa ngazi za chini hususani mabalozi na viongozi wa mashina kwani wao ndiyo wako karibu na wanachama kwani ili kushinda uchaguzi kwani ndiyo malengo ya chama chochote.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Said Kanusu alisema kuwa anashangazwa na watu kutoa maneno kuwa eti bandari imeuzwa wapinzani wameishiwa hoja.

Kanusu alisema kuwa wananchi wawe na imani na wasikatishwe tamaa na wanaoleta hoja zisizo na msingi ajenda ya nchi ni kuleta maendeleo na miradi.

Naye Diwani wa Kata ya Mtambani Godfrey Mwafulilwa alisema kuwa kauli mbiu hiyo ni kuimarisha ngazi ya chini ya mabalozi kuwapa nguvu kwani wanakazi kubwa kukiimairisha chama.

Mwafulilwa alisema kuwa ngazi ya msingi sana ni balozi ambapo chama kinarudi chini ambako huko ndiko kwenye wanachama na hoja za wanachama na wananchi.

Alisema kuwa Rais ni mvumilivu na hawavutiwi na tabia inayofanywa na watu wanamchafua wao wanapaswa kuja na hoja na ushauri ila siyo kumchafua.

No comments:

Post a Comment