Sunday, August 20, 2023

CCM WAASWA KUFUATA UTARATIBU

 

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani wanaotoa misaada na kufanya shughuli za maendeleo wametakiwa kufuata utaratibu ili kuepusha mkanganyiko na viongozi waliochaguliwa na wananchi.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa Hamoud Jumaa wakati wa mkutano wa tathmini baada ya ziara ya CCM Kibaha Mjini.

Jumaa alisema kuwa kukisaidia chama siyo tatizo lakini kinachotakiwa ni utaratibu kufuatwa ili kusitokee tofauti baina ya wale wanaosaidia na wale waliochaguliwa.

"Tunajua kwa sasa ni kipindi cha kuelekea uchaguzi mwakani ni wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa na 2025 ni uchaguzi mkuu hivyo wanaotoa misaada ndani ya chama wafuate taratibu lakini siyo kosa kukisaidia chama,"alisema Jumaa.

Alisema chama kinasaidiwa na wanachama na wadau mbalimbali wana haki ya kufanya hivyo ili mradi wazingatie utaratibu uliowekwa na chama wa namna ya kuchangia.

"Chama kinajengwa na wanachama na wanaokichangia siyo tatizo hata mimi kwenye eneo langu nachangia lakini kwa kufuata utaratibu hivyo na wengine wafuate utaratibu wa chama,"alisema Jumaa.

Kwa upande wake mwentekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka alisema kuwa utekelezaji wa ilani umefanyika kwa asilimia zaidi ya asilimia 90 ndani ya kipindi cha miaka miwili tu.

Nyamka alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Kibaha fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo miradi mingi inaendelea na mingine imekamilika.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa kwa kushirikiana na serikali na wananchi wameendelea kukabili changamoto kwenye jimbo hilo.

Koka alisema utekelezaji wa ilani unaendelea vizuri na hakuna kilichokwama kila kitu kinakwenda vizuri lengo likiwa ni kuwaondolea changamoto wananchi na kutimiza malengo ya Rais.

Naye mwenekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Focus Bundala alisema kuwa wanaishukuru serikali kutoa kwa kuipatia Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 8.

Bundala alisema kuwa baadhi ya fedha zimetumika kwenye ujenzi wa shule sita za sekondari na shule tisa za msingi na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na barabara, maji na afya.

No comments:

Post a Comment