Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo amewataka askari wa Polisi Chalinze kutokuwa na muhali kwa madereva wanaokiuka Sheria za usalama barabarani.
Kauli hiyo imetolewa Leo Agosti 16 akiwa katika siku ya pili ya ziara ya ukaguzi katika Wilaya zilizopo Mkoa wa Pwani ambapo alizungumza na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali akiwataka kutokuacha jukumu la ukamataji wa madereva wanaovunja Sheria kwa askari wa kikosi cha usalama barabarani pekee,badala yake nao wachukue hatua ili kuweza kutokomeza ajali za mara kwa mara zinazotokana na makosa ya kibinadamu kama vile kuyapita magari mengine bila tahadhari, mwendo kasi, matumizi ya vileo na kutokuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu.
Hivi karibu watu wa nne wa familia moja walipoteza maisha katika ajali ya barabarani eneo la Mapatano, Kata ya Mbwembwe tukio ambalo lilivuta hisia kwa watu wengi kutokana na ajali hiyo ya barabarani.
Kamanda Lutumo amesema " Askari wote wana jukumu la kutoa taarifa kwa wenzao waliopo barabarani pindi wanapoona dereva anaendesha gari kwa kuvunja Sheria za usalama barabarani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa".
Aidha, amewakumbusha umuhimu wa utoaji huduma bora pindi wanapowakamata madereva wanaovunja Sheria kwa kuwaeleza makosa yao kabla ya kutoa adhabu ili wajue makosa yaliyopelekea kupewa adhabu husika.
No comments:
Post a Comment