Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga alipozungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.
Mlenga alisema kuwa baada ya bunge kufanya marekebisho sheria inaruhusu wadai kukubaliana nje ya mahakama kwa maridhiano ya pande mbili na kumaliza shauri kisha kufutwa na mahakama.
"Tunawashauri wananchi watumie vituo hivi ili kutatua mashauri ya madai nje ya mahakama endapo watakubaliana na makubaliano hayo yatasajiliwa na mahakama na kuimaliza kesi hiyo,"alisema Mlenga.
Alisema kuwa faida ya kumaliza mashauri ya madai nje ya mahakama ni kuokoa muda na hakutakuwa na uadui baina ya pande hizo mbili tofauti na kuendesha kesi mahakamani.
"Njia hii ya usuluhishi na upatanishi ni nzuri kwani ni rafiki na haina uhasama ambapo kesi inapofanywa mahakamani kunakuwa na uhasama sana hivyo wananchi watumie fursa hii,"alisema Mlenga.
Aidha aliwataka wananchi kutumia zaidi maridhiano katika changamoto za mashauri ya madai ambapo itaipunguzia mahakama mlundikano wa kesi hivyo kutotumia muda mrefu.
Kwa upande wake meneja wa KPC Dismas Chihwalo alisema kuwa kituo chao kinatoa huduma bure kwa watu wenye mashauri mbalimbali ya kisheria.
Chihwalo alisema kuwa wameweza kutatua changamoto nyingi za kisheria na kufanikisha wananchi kupata haki zao kwa njia usuluhishi kwenye mashauri mbalimbali.
No comments:
Post a Comment