DIWANI wa Kata ya Kibaha Goodluck Manyama amejitolea kuipatia Shule ya Msingi Jitegemee mashine ya kudurufu karatasi ili kuipunguzia mzigo shule hiyo gharama za uchapishaji mitihani.
Aidha katika kukabili changamoto ya maji kwenye shule hiyo Halmashauri itapeleka mradi wa kisima cha maji.
Akizungumza shuleni hapo wakati wa mahafali ya darasa la saba alisema kuwa atawanunulia mashine hiyo baada ya shule hiyo kutoa ombi hilo kwake.
Manyama alisema kuwa hiyo ni moja ya changamoto kubwa zinayoikabili shule hiyo hivyo ameona awapunguzie mzigo huo ili kupunguza gharama za kudurusu mitihani na kazi nyingine za shule.
"Nimeona nitoe msaada huu ili iwe chachu na kwa wadau wengine wajitokeze kusaidia changamoto za shule ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri,"alisema Manyama.
Alisema kuwa atashirikiana na wadau wengine pamoja na wanajamii kuhakikisha wanatatua changamoto za shule hiyo ili itoe elimu bora kwa wanafunzi.
"Tumepata wadau watatuchimbia kisima ili maji yawe ya uhakika na tayari mipango imekamilika na kisima kitachimbwa hivyo tuvute subira baada ya muda mfupi maji yatapatikana,"alisema Manyama.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Stori Samatta alisema kuwa katika kuhakikisha wanakabili changamoto amekuwa akishirikisha wadau kuchangia elimu shuleni hapo.
Samatta alisema kuwa licha ya kuwa na changamoto kwani baadhi ya wanajamii kutokuwa na moyo wa kuchangia lakini anawapa elimu ya kuwa na moyo wa kuchangia ili iwe faida kwa watoto wao.
Naye mwanafunzi Eveline Samweli alisema kuwa wanakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na upungufu wa maji, matundu ya vyoo, kutokuwa na uzio na chumba cha kompyuta na kompyuta.
Samweli alisema kuwa changamoto nyingine ni shule kutokuwa na jengo la utawala ambapo jumla ya wahitimu kwa mwaka huu ni 126 ambapo shule hiyo ina wanafunzi 912 na ilianzishwa mwaka 2004 na ina walimu 24.
No comments:
Post a Comment