MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezitaka Halmashauri za Mkoa huo kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ili wapatiwe mafunzo ya Mpango Mkakati wa Kuongeza Mapato ambayo ndiyo dira ya Rais na TAMISEMI.
Kunenge aliyasema hayo Mlandizi wakati akizungumza na wataalamu mbalimbali na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha alipokuwa akifungua mafunzo ya namna ya kuongeza mapato kwenye Halmashauri kupitia mpango wa miaka mitano wa Mpango Mkakati wa Kuongeza Mapato kwa kipindi cha miaka mitano ijayo mafunzo yaliyoandaliwa GIZ.
Alisema kuwa upatikanaji wa mapato mengi kutasaidia utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo na kupunguza kero kwa wananchi na hiyo itamsaidia Rais.
"Ifikie hatua Halmashauri zetu zitoe gawio kwa serikali kama ilivyo kwa mashirika ya umma ili kuisaidia ili iweze kuhudumia Watanzania hivyo wote kwenye miradi mikubwa ya nchi ikiwemo ile ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo yetu,"alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa Halmashauri zishirikiane na GIZ ili kupata mafunzo hayo kwa lengo la kuongeza mapato pia watumie teknolojia ili kukusanya mapato ambapo mapato yakiongezeka itasaidia kuipa uwezo serikali kuhudumia wananchi wake.
"Tubuni vyanzo vipya vya mapato na tusitegemee kuuza ardhi tu peke yake kwani inakwisha tubuni vyanzo ambavyo ni endelevu hususani kwenye sekta ya uwekezaji ambayo ina nafasi kubwa ya kutuinua kiuchumi ili tuweze kuongeza mchango wetu kwenye uchumi,"alisema Kunenge.
Alibainisha kuwa Halmashauri ziangilie namna ya tozo ili zisiwe kero na kusababisha kuua au kukwamisha uwekezaji ambapo mapato ni takwimu kwa kujua wanaostahili kulipa ili mkusanye kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa George Nsajigwa Mpango Mkakati huo wa Kuongeza Mapato kwa Halmashauri hapa nchini uko kwenye mikoa ya Arusha, Tanga, Pwani ambapo ndo mkoa wa kwanza kufanya mafunzo hayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana ambapo malengo yao kwa Halmashauri ya Kibaha Mji ni kufikia makusanyo ya shilingi bilioni 30 na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kukusanya bilioni 20 katika kipindi cha miaka mitano.
John alisema kuwa ili kufikia malengo hayo wameamua kuwa na mafunzo ili kuwa na mipango ya kisayansi katika ukusanyaji wa mapato pia kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ambavyo wanaamini vitawafikisha huko.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Butamo Ndalahwa alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kupata mbinu mpya za ukusanyaji wa mapato ambapo kwa mwaka jana Halmashauri hiyo iliongoza kwa ukusanyaji mapato.
Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Peter Laizer mshauri wa mradi wa utawala bora wa fedha kutoka shirika hilo alisema kuwa mafunzo hayo yatawahusisha wataalamu wa masuala ya fedha kwenye Halmashauri kushirikiana na vitengo vingine.
No comments:
Post a Comment