MKURUGENZI wa benki ya APSA Nechi Msuya (45- 50) mkazi wa Dar es Salaam na watu wengine watatu wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga gari lingine uso kwa uso.
Akizungumza na waandishi wa habari wa ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema watu hao walifariki papo hapo.
Lutumo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 2.30 kijiji cha Mapatano Kata ya Mbwewe wilaya ya kipolisi chalinze.
Alisema kuwa marehemu alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Prado lenye namba za usajili T 104 CBU likitoka Dar es Salaam kwenda Same mkoani Kilimanjaro.
"Gari lake liligongana na lori lenye namba T 881 DWU na tela namba T 888 DWU aina ya Scania likitoka Arusha kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na Philipo Mtisi (43) mkazi wa Mafinga,"alisema Lutumo.
Aliwataja watu wengine waliokufa kuwa ni Dayana Mgeta (40-45) mfanyabiashara, Nora Msuya (40-45) mwalimu wa chuo kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam na abiria wa kike ambaye jina lake bado halijafahamika (30-35).
Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Prado kuhama upande wake wa kushoto wa barabara kwenda upande wa kulia kisha kugongana uso kwa uso na lori hilo.
Aidha alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye zahanati ya Lugoba kwa uchunguzi na kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi baada ya uchunguzi.
"Tunawashauri watumiaji wa barabara wakiwemo wale wanaotumia vyombo vya moto kuwa makini ili kupunguza ajali ambazo zinazuilika,"alisema Lutumo.
No comments:
Post a Comment