Tuesday, August 22, 2023

MAKAM WA RAIS DK MPANGO ATAKA WAKUU WA MIKOA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI





MAKAMU wa Rais wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Philip Mpango ameitaka mikoa nchini kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo mabaraza ya biashara ya mikoa na kutowatumia wakati wa kuomba michango ya shughuli za maendeleo.

Dk Mpango aliyasema hayo jana Mjini Kibaha kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa mikoa na makatibu Tawala wa mikoa Tanzania Bara.

Alisema kuwa baadhi ya sekta hiyo imeikitumika na kuwa nao karibu wanapokuwa wanahitaji michango kutoka kwao ikiwemo ya mbio za mwenge, ugeni na maadhimisho mbalimbali.

"Mnapaswa kuwa karibu na sekta binafsi na mabaraza ya biashara ya mikoa yenu kwani ni wadau muhimu wa maendeleo na wakifanya vizuri watatoa ajira kwa watu wengi hivyo lazima muwashirikishe na kuwa karibu nao kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo,"alisema Dk Mpango.

Alisema kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa wamekuwa na mahusiano mabaya na waliochini yao na wengine hujihusisha unyanyasaji wa kijinsia, kuwa wababe na upendeleo kwenye upandishwaji vyeo.

Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki alisema kuwa mafunzo hayo ni maelekezo ya Rais kutaka viongozi wapewe mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo ili kuboresha utendaji kazi wao.

Kairuki alisema kuwa mafunzo hayo ni kama waliofanyiwa wakuu wa Wilaya 139 huko Dodoma Machi mwaka huu, mafunzo kwa maofisa tarafa na watendaji wa kata 356 kwenye mikoa ya Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa na yatafanywa ya wakurugenzi Septemba mwaka huu.

Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete aliyemwakilisha waziri George Simbachawene alisema kuwa kundi hilo ni muhimu sana kwani asilimia 70 ya viongozi hao ndiyo wanaosimamia masuala mazima ya maendeleo.

Kikwete alisema kuwa viongozi hao wanaliwakilusha Taifa kwenye sera zote za serikali kupitia mamlaka za mikoa na serikali za mitaa hivyo watahakikisha kunakuwa na tija kwenye ofisi za umma kuwa na utawala bora na maadili kwa utumishi wa umma.


No comments:

Post a Comment