Monday, August 7, 2023

BILIONI 157.5 ZATUMIKA UNUNUZI BIDHAA ZA AFYA

 

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa fedha kwa Bohari ya Dawa Tanzania ambapo kiasi cha shilingi bilioni 157.5 kwa mwaka wa fedha 2022/23 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya za vituo vya kutolea huduma za afya ikijumuisha Dawa,  Vifaa Tiba na vitendanishi vya Maabara.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Hassan Ibrahim ambaye ni Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini amesema hayo leo Agost, 7, 2023 Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari alielezea utekelezaji wa majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD) na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/24.

Ibrahim amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23 Bohari imeanza kusambaza Dawa kwa mizunguko mara sita kwa mwaka kutoka Mara nne kwa mwaka huku Akisema serikali imetoa ahadi ya kuipatia MSD mtaji ili kumaliza changamoto zinazoikabili Taasisi hiyo.

Katika kufanikisha ongezeko la uzalishaji wa bidhaa za afya nchini na kuendana na azma ya Serikali ya uanzishaji wa viwanda, MSD ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miundombinu ya kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi mkoani Njombe na kuanza uzalishaji ndani ya mwaka huu wa fedha 2023/24. 

Amesema katika mwaka huu wa fedha wa 2023/24, MSD inatarajia Kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuboresho matumizi ya takwimu za maoteo, kuhakikisha bidhaa zote za afya zinakuwa na mikataba ya muda mrefu na kuimarisha ushirikiano na wazalishaji wa ndani kwa kutoa fursa kwa wazalishaji wa ndani na kununua kutoka kwa wazalishaji wa nje pale inapobidi.

Kwa upande wake Michael Bajile Meneja Maoteo Ametoa wito kwa watoa huduma za Afya kuwa makini katika takwimu wanazozikusanya kwani Bohari ya Dawa huzalisha kufuata takwimu hizo.

No comments:

Post a Comment