WANAFUNZI Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kuzingatia maadili wanayofundishwa shuleni na kutojiingiza kwenye vitendo viovu vya utovu wa nidhamu.
Hayo yamesemwa na msaidizi wa sheria kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) Dominika Ndumbaro alipokuwa akifundisha somo la sheria ya mtoto kwenye shule ya sekondari ya Mwambisi.
Ndumbaro amesema kuwa ili kuepukana na vitendo vya ukatili ambavyo wanafanyiwa wanafunzi wanapaswa kutojiingiza kwenye vitendo viovu vinavyosababisha ukatili.
Amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakishiriki vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya kama uvutaji bhangi, unywaji wa pombe, kwenda disko au sehemu za starehe.
Aidha alisema kuwa huko wanakutana na watu waliowazidi umri hivyo kuwafanyia vitendo vikiwemo vya ubakaji, ulawiti na hata vipigo endapo hawata sikiliza matakwa yao.
Aliongeza kuwa wanafunzi wanapojiingiza kwenye hali hiyo hushindwa kusoma na kujikuta wakiwa watoto wa mitaani na kujifunza wizi na kujiuza hivyo kutomaliza masomo yao.
Aliitaka jamii kwa kushirikiana na walimu na viongozi kukabili vitendo viovu kwa kuwahimiza wanafunzi kuwa na maadili mema na kumtanguliza Mungu ili kuepukana na vitendo hivyo.
Kituo cha Msaada wa Sheria kinanajihusisha na utoaji wa elimu ya sheria kwa masuala yote ya kisheria pia kinatoa msaada wa sheria kwa watu wenye changamoto za kisheria.
No comments:
Post a Comment