Wednesday, August 16, 2023

TAKUKURU PWANI YABAINI MIRADI KAMATI HEWA MIRADI YA HALMASHAURI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imebaini uwepo wa kamati hewa kwenye baadhi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Takukuru Mkoa huo Christopher Myava alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Myava alisema kuwa kutokana na kamati hewa kunasababisha mianya ya rushwa katika malipo yanayofanyika.

"Pia tumebaini kuwa jamii kutokuwa na umiliki wa miradi hiyo kutokana na kutoshirikishwa katika utekelezaji wake mfano ujenzi wa kituo cha afya Kisiju ambapo jamii haikushirikishwa kabisa,"alisema Myava.

Alisema kuwa mradi mwingine ambao ulibainika kuwa na changamoto ni mzabuni aliyechaguliwa kupeleka vifaa vya ujenzi shule ya sekondari ya kata ya Shungubweni hakuomba kazi hiyo kwenye mfumo wa serikali wa TANEPS.

"Mzabuni huyo alipewa zabuni kinyume cha utaratibu na tukafanya kikao na Halmashauri kwa lengo la kuhakikisha waombaji wa zabuni wanashindanishwa ili kuondoa dhana ya utoaji zabuni kwa upendeleo,"alisema Myava.

Alibainisha mradi mwingine ni kwenye soko la Mnarani Halmashauri ya Mji Kibaha wakusanyaji wa ushuru kutotoa risiti za mashine EFD baada ya wafanyabiashara kufanya malipo kwa kisingizio cha ubovu wa mashine.

"Sababu nyingine wanasema kuwa eti mashine haina chaji hali ambayo imesababisha wakusanyaji kutumia fedha hizo kwa matumizi yao binafsi,"alisema Myava.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo kunakosekana kumbukumbu za wafanyabiashara waliofanya malipo hivyo kusababisha upotevu wa mapato.

"Maegesho ya magari nako kuna upotevu wa mapato unaosababishwa na utendaji mdogo wa kukusanya mapato ambapo baadhi ya wakusanyaji hutoza viwango tofauti vya ushuru kwa malori yanayoegeshwa sokoni tofauti na vilivyowekwa kwenye sheria ndogo,"alisema Myava.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Pwani alisema kuwa baada ya kubaini hayo walifanya kikao na wadau wa soko na kuweka maazimio ikiwa ni pamoja na kudai risiti, kutoa taarifa za ubovu wa mashine na kuweka vibao vinavyoonyesha tozo.

No comments:

Post a Comment