Friday, August 18, 2023

DKT KIJAJI AWATAKA WAFANYABIASHARA KUJENGA MIUNDOMBINU YA UWEKEZAJI

 


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kujenga miundombinu wezeshi kwa wawekezaji na wageni  kwani baada ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko la wageni kutoka sehemu mbalimbali Duniani.

Kijaji ameyasema hayo leo Agosti 17, 2023 wakati wa Kikao kazi na wafanyabiashara wa Jiji la Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa ambapo kikao hicho kimewahusisha wajasiriamali na wafanyabiashara pamoja na majukwaa yanayojihusisha na ujasiriamali. 

Waziri Kijaji amesema uchumi imara wa Taifa upo mikononi wa sekta binafsi hivyo amewahimiza wafanyabiashara hao kutumia fursa zote zinazojitokeza  iwe ni sekta binafsi au kutoka serikalini ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi. 

Waziri Kijaji amewahimiza wajasiriamali kuwa waaminifu na Fedha zinazotolewa na Serikali kama sehemu ya mtaji ili kuwawezesha na wengine kupata hiyo fursa. 

"Lazima tukubaliane na utaratibu uliowekwa uadilifu wetu, uaminifu wetu ni muhimu hakuna fedha za bure sehemu yeyote lazima uwe na uhakika wa fedha kurudi  na mtu unae mpatia fedha hivyo tunatakiwa kumthibitishia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo mtetezi wetu namba moja "ameeleza Kijaji

Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akitoa salamu za Mkoa amempongeza Waziri huyo kwa kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao pamoja na kutatua changamoto na kero  zilizokuwa kikwazo katika utekelezaji wa biashara zao.

Senyamule amesema Mkoa wa Dodoma upo tayari kupokea wawekezaji na kuongeza idadi ya viwanda ili kuongeza na kukuza mapato ya Serikali na uchumi wa nchi ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment