Naibu Waziri Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema dhamira ya maonyesho ya wanyama wafugwao ni kutambua mchango na juhudi za wafugaji katika kuchangia maendeleo ya Taifa na mtu mmoja mmoja.
Silinde amesema hayo katika viwanja vya Ranchi ya Taifa vilivyopo katika maonyesho ya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi rasmi wa maonyesho ya Mifugo ambayo maonyesho hayo huambatana na mashindano ya kushindanisha na kumpata mfugaji aliyefuga kwa tija na mafanikio katika Mifugo yake.
“Mashindano haya hufanyika katika nchi mbalimbali yakiwa na lengo la kutambua mchango na juhudi za wafugaji katika kuchangia maendeleo ya Taifa na mtu binafsi na huongeza ari kwa wananchi kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia”,amesema Silinde.
Aidha Mhe. Silinde amesema kuwa kuendelea kufanyika kwa maonesho na mashindano hayo kunachangia na kuhamasisha kuendeleza ufugaji bora nchini.
“Wizara inaangalia namna ya kufanya maonesho haya kuwa na Taswira na hadhi ya Kitaifa kama ilivyokusudiwa na wafugaji wa walioshinda katika Kanda mbalimbali watakuja Dodoma kushindana hapa Kitaifa hivyo Wizara itaendelea kuboresha tuzo na zawadi kwa washindi ili kuwapa hamasa zaidi”, amedokeza Mhe. Silinde.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema Mkoa wake unashika nafasi ya tano Kitaifa kwa kuwa na Mifugo Mingi hivyo hawana budi kuimarisha juhudi za kukuza uchumi wa wananchi wa Mkoa huo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoyumbisha uzalishaji wenye tija.
“Kwa mujibu wa sensa ya kilimo ya mwaka 2021 mkoa wa Dodoma unashika nafasi ya 5 kwa wingi wa ng’ombe ukikadiriwa kuwa na ng’ombe 2,195,576, mbuzi 1,663,483 na wanyama wengine wafugwao hivyo juhudi zozote za kuimarisha uchumi wa wananchi wa Mkoa huu ni kipaumbele chetu, hatuna budi kushughulikia changamoto mbalimbali zinazosababisha tija ndogo katika uzalishaji wa mazao na Mifugo”,amesema Senyamule.
Maonyesho hayo ya wanyama yanafanyika kwa mara ya 12 tangu kuanzishwa kwake hufanyika katika Kanda mbalimbali na baadae hutamatishwa kwa kunganishwa Kanda zote na mshindi hupatikana akiwa ndiye mshindi wa Taifa na hupatiwa zawadi na motisha kutoka wizara ya Mifugo na Uvuvi.
No comments:
Post a Comment