Sunday, March 29, 2026

KITUO CHA WANAWAKE WAJASIRIAMALI MANISPAA YA KIBAHA KUJENGA KIWANDA CHA KUTENGENEZEA BATIKI

NGUO za Batiki zimekifanya Kituo cha Wanawake Wajasiriamali Manispaa ya Kibaha kuitangaza Tanzania kwenye soko la Kimataifa ambapo ziliongoza kwa kununuliwa kwenye maonyesho nchi jirani. 

Akizungumza ofisini kwake Mjini Kibaha Mwenyekiti wa Kituo hicho Dk Magdalena Mangi alisema kuwa walishirki maonyesho kwenye nchi za Sudan, Kenya na Burundi miaka ya hivi karibuni ambapo zilinunuliwa kwa wingi.

Mangi alisema kufuatia batiki zao kuwa na soko kubwa wamejipanga kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa batiki ili kuongeza ubora wa bidhaa hiyo ili kuendelea kuitangaza nchi wanapokwenda kwenye maonyesho kama hayo siku za baadaye kwani wamedhamiria kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Mangi alisema kuwa kwa sasa wanazalisha batiki kwa kutumia mikono hali inayofanya ubora kupungua lakini wanaamini wakitumia mashine wataongeza ubora.

"Batiki tunazozalisha ni nzuri kwani tunatumia vitamba vizito ambavyo havichuji tofauti na wazalishaji wengine hali ambayo inatufanya tupate soko maeneo mbalimbali ambapo ushiriki kwenye nchi Burundi mwaka 2023, Sudan Kusini 2024, na Kenya 2025  tulipata mafanikio makubwa,"alisema Mangi.

Alisema kuwa wamekuwa wakipata masoko maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na watu binafsi na taasisi zikiwemo za watu binafsi na za serikali.

"Tuna soko japo siyo kubwa sana lakini tunataka tujitanue kwa kujitangaza kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii ili kuwafikia wateja wengi,"alisema Mangi.

Aidha alisema kuwa changamoto inayowakabili ni mtaji ambapo wakipata fedha watahakikisha wanajenga kiwanda ili kuongeza ubora wa batiki zao.

"Tulikopa Halmashauri kiasi cha shilingi milioni 40 ambapo bado tunaendelea na marejesho na tunahitaji sehemu ya kutengenezea batiki kwani hapa eneo ni dogo hali inayofanya tutengenezee nyumbani,"alisema Mangi.

Aliongeza kuwa wanaishukuru serikali kwa kuendelea kuwawezesha ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na kuwawezesha hata kwa mikopo ya asilimia 10 ili kukuza biashara zao.

Naye Simon Kiondo mkufunzi wa masuala ya fedha na ujasiriamali alisema kuwa alikipatia elimu ya biashara mtandaoni ili kupata masoko zaidi kwani hiyo ni moja ya njia za kuongeza wateja.

Kiondo alisema kuwa baadhi ya changamoto ya vikundi vya ujasiriamali ni kukosa mipango na malengo na utunzaji wa kumbukumbu na ukosefu wa elimu ya fedha.

Alisema kuwa wajasiriamali wanapaswa kujitangaza na kwenda na wakati kwa kutumia teknolojia ya kisasa kupitia mitandao ya kijamii kuvutia masoko.

Kituo hicho kina jumla ya wanachama 10 na kinajohusisha na uzalishaji wa batiki, sabuni, mafuta mbalimbali, urembo, ushonaji nguo na khanga.

Thursday, March 26, 2026

PROGRAM YA MALEZI MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO YAPATA MAFANIKIO






PROGRAM ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto imeleta manufaa makubwa kwa kuanzishwa kadi ya alama kwa watoto inayorahisisha ufuatiliaji.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Shirika lisilo kuwa la Kiserikali la Anjita Child Development Foundation Janeth Malela wakati wa kikao cha wadau wa Program hiyo Mkoa wa Pwani.

Malela amesema kuwa kuanzishwa kwa kadi hiyo kwa watoto ni mafanikio makubwa ya Program hiyo katika kuhakikisha ustawi wa watoto katika makuzi yake.

Amesema kuwa kikao hicho kiliweza kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya uchechemuzi wa umuhimu wa kuwekeza kwenye Program hiyo na kusaidia serikali kutekeleza Program za malezi.

"Kuendelea kushirikiana na wadau wa nje katika kuwekeza katika malezi kuhamasisha jamii na serikali katika kuanzisha vituo vya kulea watoto wadogo mchana vya jamii,"amesema Malela.

Msajili wa mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Elia Kabora amesema kuwa uwekezaji kwa watoto ni moja ya vipaumbele ili kuhakikisha makuzi ya watoto yanazingatia upatikanaji wa huduma muhimu.

Kabora amesema kuwa Programu hiyo inalenga kuimarisha utoaji huduma bora za Afya, Lishe, Malezi yenye Mwitikio, ujifunzaji wa Awali na Ulinzi na Usalama kwa watoto wa miaka 0 hadi 8 na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa sekta mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika yasiyo kuwa ya Kiserikali Kibaha Mjini (KITAN) Dk Rose Mkonyi amesema kuwa jamii kwa kushirikiana wadau wengine wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji muhimu ili waweze kupata huduma muhimu.

Mkonyi amesema kuwa wadau wanapaswa kuungana kufanikisha Program hiyo ili kuweza kufanikisha ukuaji na maendeleo ya mtoto kikamilifu kimwili, kiakili, kukuza lugha, mawasiliano kijamii na kihisia. 

Walengwa wa mradi huo walioshiriki kikao hicho ni pamoja na wazazi, walezi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, viongozi wa dini na wataalam wa ngazi ya serikali.

mwisho.

Sunday, March 22, 2026

UKUWAWAVI WATOA MISAADA KITUO CHA YATIMA BULOMA


UMOJA wa Kusaidiana Wanajeshi Wastaafu wa Vifaru (UKUWAWAVI) wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwenye Kituo cha Kulea Yatima cha Buloma.
Wametoa misaada hiyo ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Iddi el Fitri na Mfungo wa Kwaresma.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi misaada hiyo Mwenyekiti wa (UKUWAWAVI) SSGT Omari Makore amesema kuwa wameguswa kuwasaidia watoto hao ili nao waweze kufurahi kama walivyo watoto wanaoishi na familia zao.

Makore amesema wanajua kuwa watoto hao wana mahitaji mengi lakini wameona
waanze na kidogo walichojaliwa na hiyo ni sadaka na wataendelea kusaidia pale watakapojaliwa wakati mwingine.

"Tutarudi tena kwani watoto hawa wametuonyesha mapenzi makubwa na huu ni mfano na vikundi na watu mbalimbali nao wajitokeze kuwasaidia watoto hawa,"amesema Makore.

Kwa upande wake Mlezi wa (UKUWAWAVI) Brigedia Jenerali Rajabu Hanti (Mstaafu) amesema kuwa watoto hao ni Taifa la kesho wanahitaji malezi ya watu.

Hanti amesema kuwa watoto hao wanapaswa kupelekewa furaha kwa kuwashika mkono kwa misaada mbalimbali ambayo ni mahitaji yao ya msingi.

Naye Mchungaji Jackson Bukelebe amesema kuwa umoja huo umechukua jukumu la kidini kwani dini bora ni ile inayojali yatima watu wanapaswa kujotolea kuwasaidia watoto hao.

Mwasisi wa kituo hicho Anna Kyando amesema kuwa wanashukuru kwa misaada hiyo kwani wadau ndiyo wamekuwa wakiendesha kituo hicho kwani bila wao peke yake asingeweza.

Kyando amesema kuwa changamoto kubwa ni chakula kwani ndicho kinachohitajika muda wote uzio wa ukufa, vifaa vya shule, ada kwa wanafunzi walioko vyuoni kutoka kituo hicho.

Moja ya watoto wa kituo hicho Yohana Almas amesema kuwa wanashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kufanya vizuri kwenye masomo yao na kuomba watu waendelee kuwasaidia.

Baadhi ya vitu vilivyotolewa ni pamoja na mchele kilo 100, unga wa sembe kilo 50, maharage kilo 50, mafuta lita 20, madaftari 100, juisi katoni 5, maji katoni 10, doti 5 za khanga, sabuni za unga, taulo za kike na biskuti.

Saturday, March 21, 2026

DA ARUL ARQAM LEARNING CENTRE (DAALC) KUJENGA HOSPITALI YA KISASA.

TAASISI ya DA ARUL ARQAM LEARNING CENTRE (DAALC) ya Kibaha Mkoani Pwani inatarajia kujenga kituo cha taasisi chenye huduma mbalimbali za kijamii kikiwa ni pamoja Hospitali ya kisasa kwa gharama za shilingi bilioni 5.5.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwalimu wa Taasisi hiyo Karume Amri Abeid amesema kuwa kituo hicho kitajengwa eneo la Boko Wilaya ya Kibaha.

Abeid amesema kuwa eneo hilo ndilo litakalokuwa makao makuu ya Taasisi ambalo lina ukubwa wa hekari 11 na tayari nyumba ya mlinzi tayari imejengwa kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi.

"Eneo hilo pia kutajengwa ofisi, Msikiti, shule ya awali hadi elimu ya juu yaani kidato cha sita, chuo cha elimu ya dini Ibtidai mpaka Thanawi, kituo cha kuhifadhisha Quran kwa watoto kuanzia miaka 5 na kuendelea,"amesema Abeid.

Amesema kuwa njia watakayoitumia kupata fedha ni michango mbalimbali toka kwa wadau, waumini na kufanya harambee ambapo hadi sasa wamekusanya kiasi cha shilingi milioni 2.

"Huduma zikiwemo za afya zitatolewa kulingana na jinsi badala ya huduma kutolewa na jinsi tofauti na wanufaika kwenye sekta ya afya na ajira haitajali dini bali ni kwa dini zote kwani lengo ni kutoa huduma bora na za kisasa,"amesema Abeid.

Aidha amesema kuwa matarajio ni kuanza ujenzi Januari mwakani mara fedha zitakapopatikana na kikubwa wadau mbalimbali wajitokeze kuchangia fedha ili kufanikisha ujenzi huo kwani watu wajitoe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kujenga ahera yetu.

Akizungumzia kuhusu sikukuu ya Iddi amesema kuwa siyo kuvaa vizuri na kupendeza bali ni kwa yule mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na kukumbuka siku ya hesabu (Kiyama) ndiyo maana ya Iddi.

Ameongeza kuwa watu wamwabudu Mwenyezi Mungu na kuacha kumkasirisha na waishi maisha haya na si wakati wa mfungo peke yake ili wasimkosee.

DA ARUL ARQAM LEARNING CENTRE (DAALC) KUJENGA HOSPITALI YA KISASA.

TAASISI ya DA ARUL ARQAM LEARNING CENTRE (DAALC) ya Kibaha Mkoani Pwani inatarajia kujenga kituo cha taasisi chenye huduma mbalimbali za kijamii kikiwa ni pamoja Hospitali ya kisasa kwa gharama za shilingi bilioni 5.5.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwalimu wa Taasisi hiyo Karume Amri Abeid amesema kuwa kituo hicho kitajengwa eneo la Boko Wilaya ya Kibaha.

Abeid amesema kuwa eneo hilo ndilo litakalokuwa makao makuu ya Taasisi ambalo lina ukubwa wa hekari 11 na tayari nyumba ya mlinzi tayari imejengwa kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi.

"Eneo hilo pia kutajengwa ofisi, Msikiti, shule ya awali hadi elimu ya juu yaani kidato cha sita, chuo cha elimu ya dini Ibtidai mpaka Thanawi, kituo cha kuhifadhisha Quran kwa watoto kuanzia miaka 5 na kuendelea,"amesema Abeid.

Amesema kuwa njia watakayoitumia kupata fedha ni michango mbalimbali toka kwa wadau, waumini na kufanya harambee ambapo hadi sasa wamekusanya kiasi cha shilingi milioni 2.

"Huduma zikiwemo za afya zitatolewa kulingana na jinsi badala ya huduma kutolewa na jinsi tofauti na wanufaika kwenye sekta ya afya na ajira haitajali dini bali ni kwa dini zote kwani lengo ni kutoa huduma bora na za kisasa,"amesema Abeid.

Aidha amesema kuwa matarajio ni kuanza ujenzi Januari mwakani mara fedha zitakapopatikana na kikubwa wadau mbalimbali wajitokeze kuchangia fedha ili kufanikisha ujenzi huo kwani watu wajitoe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kujenga ahera yetu.

Akizungumzia kuhusu sikukuu ya Iddi amesema kuwa siyo kuvaa vizuri na kupendeza bali ni kwa yule mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na kukumbuka siku ya hesabu (Kiyama) ndiyo maana ya Iddi.

Ameongeza kuwa watu wamwabudu Mwenyezi Mungu na kuacha kumkasirisha na waishi maisha haya na si wakati wa mfungo peke yake ili wasimkosee.

Thursday, March 12, 2026

KIVUKO MKOMBOZI WANAFUNZI SHULE YA MAMLAKA

 MTAA wa Machinjioni Kata ya Tangini umeishukuru Serikali kwa ujenzi wa kivuko kwenye barabara inayoelekea Shule ya Msingi Mamlaka kwa kuwaondolea adha ya wanafunzi kuvuka kwa kubebwa mgongoni.

Ujenzi wa kivuko hicho ambacho kimewekwa makalavati mawili kimeweza kuwaondolea adha wanafunzi wa shule hiyo ambapo kipindi cha mvua walishindwa kuvuka hadi wavushwe na watu wazima. 

Akizungumza na Mwenyekiti wa Mtaa huo Aidan Mchiwa amesema kuwa mbali ya changamoto iliyokuwepo kwa wanafunzi lakini pia iliwakumba wakazi wa maeneo karibu na shule hiyo.

Mchiwa amesema kuwa manufaa ya kivuko hicho yameonekana ambapo mvua kubwa zilizonyesha juzi wanafunzi na wananchi wanavuka bila ya shida yoyote tofauti na ilivyokuwa awali ikiwa ni wakati wa siku 100 za Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

"Eneo hilo ni mkondo wa maji hivyo mvua zinazonyesha maeneo mbalimbali maji yake yanapita hapo kwani ni eneo ambalo kuna bonde hivyo maji yanakuwa mengi na kusababisha adha kwa watu wanaopita kwenye barabara hiyo inayoelekea shuleni,"amesema Mchiwa.

Amesema kuwa serikali kupitia Halmashauri ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 9 na kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kujenga kivuko hicho ambapo hata magari na pikiiki yalikuwa yakipita kwa shida.

"Kuna maboresho kidogo yanatakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na mitaro na tukifanikiwa kupata fedha tutaichimba kwani bajeti tuliyopewa ya ujenzi wa kivuko hicho iliisha tutaomba kwa bajeti hii ili tuboreshe zaidi,"amesema Mchiwa.

Aidha amesema kuwa pia kwa kushirikiana na wananchi walifungua barabara tatu za Aidan, Nida na Kilima huku mbili zikiwa zimebakia za kwa Kapungu na kwa Landa.

KIVUKO MKOMBOZI WANAFUNZI SHULE YA MAMLAKA

MTAA wa Machinjioni Kata ya Tangini umeishukuru Serikali kwa ujenzi wa kivuko kwenye barabara inayoelekea Shule ya Msingi Mamlaka kwa kuwaondolea adha ya wanafunzi kuvuka kwa kubebwa mgongoni.

Ujenzi wa kivuko hicho ambacho kimewekwa makalavati mawili kimeweza kuwaondolea adha wanafunzi wa shule hiyo ambapo kipindi cha mvua walishindwa kuvuka hadi wavushwe na watu wazima. 

Akizungumza na Mwenyekiti wa Mtaa huo Aidan Mchiwa amesema kuwa mbali ya changamoto iliyokuwepo kwa wanafunzi lakini pia iliwakumba wakazi wa maeneo karibu na shule hiyo.

Mchiwa amesema kuwa manufaa ya kivuko hicho yameonekana ambapo mvua kubwa zilizonyesha juzi wanafunzi na wananchi wanavuka bila ya shida yoyote tofauti na ilivyokuwa awali ikiwa ni wakati wa siku 100 za Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

"Eneo hilo ni mkondo wa maji hivyo mvua zinazonyesha maeneo mbalimbali maji yake yanapita hapo kwani ni eneo ambalo kuna bonde hivyo maji yanakuwa mengi na kusababisha adha kwa watu wanaopita kwenye barabara hiyo inayoelekea shuleni,"amesema Mchiwa.

Amesema kuwa serikali kupitia Halmashauri ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 9 na kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kujenga kivuko hicho ambapo hata magari na pikiiki yalikuwa yakipita kwa shida.

"Kuna maboresho kidogo yanatakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na mitaro na tukifanikiwa kupata fedha tutaichimba kwani bajeti tuliyopewa ya ujenzi wa kivuko hicho iliisha tutaomba kwa bajeti hii ili tuboreshe zaidi,"amesema Mchiwa.

Aidha amesema kuwa pia kwa kushirikiana na wananchi walifungua barabara tatu za Aidan, Nida na Kilima huku mbili zikiwa zimebakia za kwa Kapungu na kwa Landa.

Wednesday, March 11, 2026

BIDHAA SOKO LA LOLIONDO BEI NZURI

BEI ya Vitunguu kwenye Soko la Loliondo Halmashauri ya Manispaa Kibaha iko juu kutoka shilingi 130,000 hadi 250,000 kwa gunia.

Aidha viazi mbatata ambavyo ni maarufu kwa ajili ya kukaangia chipsi vimeshuka bei kutoka shilingi 140,000 hadi 70,000 kwa gunia.

Akizungumza ofisini kwake Mjini Kibaha Naibu Katibu Mkuu wa soko hilo Alex Msimbe alisema kuwa kwa sasa bidhaa nyingi bei zake hazijapanda sana bali bei iko wastani.

Msimbe alisema kuwa bei hiyo ya vitungu imeongezeka sana kutokana na kipindi hichi ndiyo bei huwa inapanda sana lakini baadaye bei hiyo itashuka.

"Bei ya tenga la nyanya  imeshuka kutoka kati ya shilingi 85,000 na 70,000 hadi 35,000 huku mchele ukiuzwa kati ya shilingi 3,000, 2,500 hadi 2,700 kwa kilo na maharage yakiuzwa kati ya shilingi 2,700 hadi 3,000 kwa kilo.

Alisema kuwa bei ya unga wa sembe ni kati ya shilingi 1,400 na 1,500 kwa kilo na ngano ni shilingi 125,000 kwa kilo 50 huku sukari ikiuzwa shilingi 3,000 kwa kilo.

"Bei za bidhaa nyingi bei hazijapanda kwani kipindi hichi ni cha baadhi ya maeneo ni mavuno na mengine ndiyo wamepanda muda siyo mrefu hivyo kutoathiri sana bei,"alisema Msimbe.

Aidha alisema kuwa kwa sasa hakuna changamoto kwenye soko hilo kwani miundombinu ikiwemo ya maji, umeme na huduma muhimu kama za vyoo zote ziko vizuri kwani wanashirikiana vizuri na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ambao ndiyo wanaowasimamia.

"Kuhusu mitaji baadhi ya wafanyabiashara wananufaika na mikopo ya Halmashauri ile ya asilimia 10 na asilimia 7,"alisema Msimbe.

Tuesday, March 10, 2026

DED GAIRO APONGEZWA UJENZI WA SHULE YA AMALI

Hawa Wazee wangu ni Wawakilishi wa wana Kijiji cha Kwipipa kata ya Rubeho.

Walituma salam zao kupitia kwa Mhe. Diwani wiki mbili zilizopita kuwa wananiita. Na leo nimekutana nao kuwasilikiza, kumbe walitaka kunipa shukrani kwa ajili ya Mradi wa Shule ya AMALI iliyojengwa kwenye Kijiji cha Kwipipa. Wameshukuru kwa Usimamizi hadi Ukamilishaji wa shule na hatimae watoto wameanza masomo

Wazee wangu hawa tulianza nao wakati tunatafuta eneo na wakatoa eneo lote la Mradi. Wametoa salamu zao kwa Maandishi, kuongea na mwisho wakatoa mbuzi.


Saturday, March 7, 2026

KIKUNDI CHA LULU YA WAJANE WAISHUKURU MANISPAA YA KIBAHA KWA MKOPO WA MILIONI 46

KIKUNDI cha wanawake cha Lulu ya Wajane kilichopo  Kongowe, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, kimeishukuru Manispaa ya Kibaha kwa kuwapatia mkopo wa shilingi milioni 46 uliowawezesha kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi, Mwenyekiti wa kikundi hicho Kanyenda Mweri amesema mkopo huo waliupata kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalum, na wamefanikiwa kuurejesha ndani ya kipindi cha miezi 11.

Amesema kikundi chao kinajishughulisha na ufugaji wa kuku wa aina mbalimbali, ambapo huuza kuku hao kwa jumla na rejareja na hivyo kuwa chanzo kikuu cha kipato kwa wanachama wake.

Aidha, amesema baada ya mafanikio waliyoyapata, kwa sasa wanatarajia kuomba mkopo mwingine ambao utawawezesha kununua mashine ya kutotolea vifaranga ili kupanua zaidi shughuli zao za ufugaji na kuongeza uzalishaji.

Kikundi hicho kimebainisha kuwa mkopo huo umewasaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao, sambamba na kutoa ajira kwa baadhi ya wananchi katika eneo lao.

PANGANI SEKONDARI WAPANDA MITI 344

SHULE ya Sekondari Pangani, Manispaa ya Kibaha imefanya zoezi la kupanda miti zaidi ya 344 katika mazingira ya shule hiyo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhimiza taasisi za elimu kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Zoezi hilo limehusisha wanafunzi, walimu pamoja na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Pangani kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Tatu Mwambala amefafanua miti hiyo ni ya kivuli na mbao ambapo miti 220 imetolewa na kitalu cha Manispaa, miti 110 kutoka Wakala wa Misitu kupitia Shule ya Sekondari Msangani II na miti 14 ya matunda imenunuliwa na shule.

Amesema miti hiyo itasaidia kukuza stadi za utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi pamoja na kuboresha mazingira ya shule.

Diwani wa Kata ya Pangani, John Katele amebainisha zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na mikakati ya kupanda miti milioni 1.5 katika mkoa huo.

Kwa upande wake Ofisa Kilimo wa kata hiyo, Omary Ngulengule ameeleza kuwa, wanafunzi wamepata elimu ya vitendo kuhusu uchimbaji mashimo na upandaji sahihi wa miti ili wawe mabalozi wa utunzaji wa mazingira katika jamii.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Stanley Amos ameeleza elimu waliyoipata itawasaidia kuhamasisha familia na jamii kupanda miti na kutunza mazingira.

MUHIMILI WA MAHAKAMA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANAWAKE KWA WAKATI

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Hawa Mchafu amesema mhimili wa Mahakama unatakiwa kuangalia uwezekano wa kushughulikia kwa karibu changamoto za Wanawake ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.

Mchafu ambaue pia ni Mbunge Vitimaalumu Mkoa wa Pwani amesema Serikali inatakiwa kuweka madawati ya jinsia na dawati la msaada wa kisheria katika Halmashauri ili Wanawake wanufaike kwa kupata ushauri wa kisaikolojia utakaosaidia kujikwamua kiuchumi kwa kushirikiana na wenza wao ili kupata kipato kwa ajili ya kujikimu na familia zao.

Ametoa angalizo hilo Machi 6 alipokuwa akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kibaha walioshiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambapo Manispaa hiyo ilifanya maadhimisho yake mjini Mailimoja.

Katika hotuba yake Mchafu amebainisha kwamba dawati la jinsia Polisi ambalo lina kazi ya kusikiliza na kutoa ushauri kwa matatizo yanayowasilishwa wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia, mashauri 461 yalipokelewa na kati ya hayo  63 yamepelekwa Mahakamani kwa ajili ya maamuzi zaidi. 

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudimu ya Bunge amesema kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kitaifa kwa Mwaka 2026 ni Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050 inahimiza kujenga uelewa kwa jamii na wadau, kuwekeza kwenye Maendeleo Jumuishi ikiwemo kutambua Haki za Wanawake na Wasichana.

Amesema lengo lingine ni kuhakikisha Haki za Wanawake na Wasichana  zinafanyiwa kazi kwa vitendo na kuleta mabadiliko ya kweli kama ilivyoainishwa kwenye nguzo za Dira 2050 . 

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kibaha Lea Lwanji amesema kwasasa wanaendelea kuratibu shughuli za wamachinga kwa kuwatambua na kuwasajili kwenye mfumo ambapo tayari wamachinga 1,112 kati yao wakes 732 wanaume 380.

Akielezea kuhusiana na uwezeshwaji kiuchumi Lwanji amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri imetenga sh. Biln 1.1 na kwamba mikopo yenye thamani ya sh.Billion 2.1 imetolewa kwa vikundi 436 na watu binafsi 21 kati ya vikundi hivyo 275 ni vya Wanawake ambao wamepata zaidi ya sh. Billion 1.

Ofisa Maendeleo huyo amebainisha kwamba Wajasiriamali wengi wamekuwa na mwamko wa kufanya biashara na wengi wanajitokeza kutafuta fursa za mitaji katika taasisi wezeshi.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa amewapongeza watumishi wanawake katika Manispaa hiyo kwa mchango wao katika ukusanyaji wa mapato uliowezesha Manispaa hiyo kushika nafasi ya pili kitaifa miongoni mwa Halmashauri 184 nchini Tanzania.

Dkt. Shemwelekwa amesema Manispaa ya Kibaha imefanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa katika ukusanyaji wa mapato baada ya kukusanya shilingi bilioni 17, huku idara ya Uhasibu na Mapato ikiongozwa na mwanamke.

Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ambapo kwa sasa imefikia shilingi bilioni 18, ikilinganishwa na awali ambapo ilikuwa ikikusanya shilingi bilioni 7.3.

WANANCHI WAMIMINIKA KLINIKI YA ARDHI KIBAHA WAOMBA SIKU ZIONGEZWE

 

WANANCHI wa Manispaa ya Kibaha wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika Kliniki ya Ardhi ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki, huku baadhi yao wakiomba muda wa utoaji wa huduma hizo uongezwe kutokana na umuhimu wake.

Wananchi hao pia wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna wanavyohudumiwa katika kliniki hiyo.

Maoni hayo yametolewa Machi 4, 2026, wakati kambi maalum ya kushughulikia masuala ya ardhi ikiendelea kwa siku ya tatu katika viwanja vya Maili Moja, Stendi ya Zamani, Manispaa ya Kibaha, ambapo wananchi wengi wameendelea kumiminika kupata huduma mbalimbali.

Mkazi wa Kibaha, Ester Joel, aliyefika katika kliniki hiyo kupata huduma ya hati, amesema ameridhishwa na huduma aliyoipata na kuomba muda wa kliniki hiyo uongezwe ili wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kuhudumiwa.

“Nimeridhika na huduma niliyoipata hapa. Kwanza nimepokelewa vizuri na nimeelekezwa namna ya kutatua changamoto yangu. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa huduma hii, ningependa siku ziongezwe hata kufikia wiki mbili,” amesema Ester Joel.

Kwa upande wake Coletha Nombo, ambaye pia alifika kupata huduma ya hati, amepongeza juhudi za Serikali kwa kuwaletea wananchi huduma hiyo karibu na maeneo yao.

Naye Ruth Kadema, mkazi wa Pangani, amesema ameridhishwa na huduma aliyoipata na kueleza kuwa amepewa maelekezo ya kufika tena siku ya Jumamosi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kupata hati yake.

“Huduma hii ni nzuri sana. Nimeridhika na nimeambiwa nije Jumamosi kuchukua hati yangu baada ya kuwasilisha taarifa zangu leo,” amefafanua Ruth.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa kambi hiyo maalum ya huduma za ardhi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi zinazohusu masuala ya ardhi, hususan umilikishwaji wa ardhi na upatikanaji wa hati.

Kambi hiyo maalum ya siku sita ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki ilianza rasmi Machi 2 na inatarajiwa kuhitimishwa Machi 7, 2026.

Friday, March 6, 2026

UMILIKI RASILIMALI KWA WANAWAKE WAPUNGUZA VITENDO VYA UKATILI

SERIKALI imeweka mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na umiliki rasilimali ili kupunguza vitendo vya ukatili kwa wanawake kuelekea Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Akizungumza wakati wa sherehe za Siku ya Wanawake Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani Hawa Mchafu amesema uwepo wa mazingira hayo unaondoa ukatili wa kijinsia.

Mchafu amesema kuwa uwepo wa usawa na kulinda kulinda haki za wanawake kuna mchango mkubwa katika suala la maendeleo.

"Usawa wezeshi hiyo ni nyenzo muhimu ili kuketa utandaji wa pamoja wa kufikia malengo ya dira ya maendeleo na kuongeza ushiriki wanawake kwenye masuala muhimu yakiwemo ya uongozi,"amesema Mchafu.

Amesema kuwa dhumuni la kuwarudisha wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni ni kutimiza ndoto zao kwani siyo wote waliopata ujauzito kwa kupenda au tamaa bali ni kutokana na mazingira wanayoishi na wengine wamepewa na ndugu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa aesma kuwa asilimia 70 ya watumishi ni wanawake menejimenti idara tano zinaongozwa na wanawake ambapo wanafanya kazi nzuri ikiwemo kwenye zoezi la ukusanyaji mapato.

Shemwelekwa amesema kuwa wamewawezesha wanawake wenye biashara ndogo ndogo kuunda vikundi ambapo walikuwa hawakopesheki lakini sasa wamekopeshwa bilioni 2 na wanarejesha vizuri.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Leah Lwanji amesema kuwa vikundi 275 vya wanawake vimekopeshwa zaidi ya bilioni 1 ikiwa ni asilimia 94. 

Lwanji amesema kuwa majukwaa yamehamasishwa kuanzishwa miradi ya kiuchumi ili waweze kujikwamua na mpaka sasa zimekopeshwa milioni 70 kwa akinamama wa majukwaa.

Moja ya kikundi ambacho ni cha mfano cha Lulu ya Wajane mwaka jana kilipata mkopo wa shilingi milioni 46 ambapo walipaswa kurejesha mkopo huo kwa miaka mitatu lakini kimeweza kurejesha ndani ya miezi 11.

Kiongozi wa kikundi hicho Kanyenda Mweri amesema kuwa fedha hizo za mikopo isiyokuwa na riba zimewasaidia kuwakwamua kiuchumi na kuweza kutoa ajira kwa wanawake wenzao.

Thursday, March 5, 2026

MAOFISA USAFIRISHAJI WATAKIWA KUUNDA VIKUNDI WAKOPE HALMASHAURI





MAOFISA Usafirishaji maarufu kama Bodaboda kwenye Mtaa wa Mwendapole B wametakiwa kuunda vikundi ili waweze kukopa vyombo vya usafiri vinavyotolewa na Halmashauri kuachana na mikopo ya taasisi za watu binafsi ambazo zina gharama kubwa.

Aidha alisema kuwa gharama za mikopo ya Halmashauri ni ndogo na marejesho yake ni madogo tofauti na mikopo ya vyombo hivyo kwenye taasisi au watu binafsi.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo Abubakar Matumla wakati wa kikao na waendesha pikipiki wa Mtaa huo na kuwa wanashindwa kufanikiwa kwa kukopa pikipiki kwa riba kubwa.

Matumla alisema kuwa gharama za kukopa pikipiki kwa watu binafsi imekuwa ikiwafanya wasifanikiwe kutokana na gharama kuwa kubwa za mikopo hiyo hivyo hujikuta wanashindwa kujiongezea kipato.

"Serikali imewawekea mazingira mazuri ya mikopo yake kwani mnauwezo wa kukopa pikipiki, bajaji na Toyo kwa gharama nafuu na unarejesha kiasi kilekile ulichokopa na hakuna riba ya mkopo unaokopa hivyo ni wakati wenu wa kujiunga na kuwa na vikundi na mtumie fursa ya mikopo pale Halmashauri fedha zipo za kutosha na vyombo vya moto vipo,"alisema Matumla.

Alisema kuwa yuko tayari kuwasimamia kuhakikisha wanapata mikopo hiyo kwani hapendi kuona waendesha pikipiki wakitaabika ili hali kuna sehemu wanaweza kukopa bila ya kuwa na marejesho makubwa pia aliwataka kutoa taarifa kwa wale wanaojihusisha na vitendo vya kiuhalifu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha pikipiki hao Abdulatif Mbonganga alisema kuwa tayari wameshaanzisha kikundi kimoja na tayari kimeshasajiliwa kikiwa kinasubiri wakati ukifika waende kukopa.

Mboganga alisema kuwa changamoto kubwa kwao ni kukosa vyombo vya usafiri hali inayowabidi kukopa vyombo hivyo kwenye taasisi za watu binafsi ambazo zinagharama kubwa na kujikuta wakitumia nguvu kubwa kwenye marejesho.

Moja ya maofisa usafirishaji Salum Msaku alisema kuwa changamoto ya uhalifu inatokana na baadhi yao kuwapa ma "day worker" hasa nyakati za usiku ambapo wanawaletea sifa mbaya.

Msaku alisema kuwa ili kudhibiti hali hiyo kila mwendesha pikpiki aendeshe pikipiki yake na siyo kumpa mtu mwingine pia wahakikishe wanavaa riflector ambazo zitawatambua kwa namba zinazoandikwa mgongoni inakuwa rahisi katika ufuatiliaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembe Saba B Nuru Awadh alisema kuwa wanapaswa kuwa na ushirikiano na kuunda vikundi vya bodaboda ili wapate mikopo nafauu.

Awadh aliwataka wajiheshimu na wasijiunge na makundi mabaya kwani Rais amewapa kipaumbele vijana katika uongozi na sehemu mbalimbali ili wawe vinara kwa utendaji kazi.

Tuesday, March 3, 2026

KAMBI SAMIA ARDHI KLINIKI YAANZA PWANI

HALMASHAURI ya Manispaa Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweka kambi ya Samia Ardhi Kliniki ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa katika kambi hiyo ya siku sita, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Rugambwa Banyika alisema kuwa kliniki hiyo inalenga kutoa ushauri wa kisheria kuhusu masuala ya ardhi.

Banyika alisema kuwa shughuli nyingine zitakuwa ni kufanya makadirio ya pango la ardhi, kuandaa nyaraka za umiliki, kujibu changamoto za upimaji, urasimishaji, upangaji miji na michoro pamoja na kutoa hati za umiliki.

"Wananchi wote wanakaribishwa ili kupata huduma zote zihusiananazo na masuala ya ardhi ambapo huduma zimesogezwa ili kila mwananchi apate fursa katika kipindi hichi kuanzia Machi 2 hadi 7 kuelekea kilele cha siku ya Wanawake Duniani Machi 8,"alisema Banyika. 

Alisema kuwa kambi hiyo maalum ina lengo la kushughulikia changamoto mbalimbali za ardhi kwa wananchi hususan wanawake na wasichana katika masuala yanayohusiana na ardhi.

Baadhi ya wananchi Mariam Juma na Ahmed Abdala wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna wanavyohudumiwa na wataalamu wa ardhi kwani wanatoa elimu ya kujitosheleza.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa kinatarajiwa kufanyika Machi 8 2026 katika Uwanja wa Ujamaa Kata ya Umwe Tarafa ya Ikwiriri Halmashauri ya Mji wa Rufiji ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Sunday, March 1, 2026

PWANI YAANZA MAANDALIZI MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

MKOA wa Pwani umeanza maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo kilele cha maadhimisho kimkoa yatafanyika Machi 8, 2026 katika Uwanja wa Ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji Rufiji. 

Mratibu wa maadhimisho hayo, Roseline Kimaro, amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.

Akizungumza kuhusu maandalizi, Kimaro amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” ikisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na haki kama nguzo ya maendeleo endelevu. 

Amesema lengo ni kutambua na kuenzi mchango wa wanawake katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Amebainisha kuwa kuanzia Machi 1 hadi 7 kutafanyika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma na kampeni za uhamasishaji kuhusu usawa wa kijinsia,  kilele cha maadhimisho Machi 8. 

Ameongeza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na kutoa wito kwa wananchi na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuunga mkono jitihada za kulinda na kuimarisha haki za wanawake na wasichana.