Tuesday, March 3, 2026

KAMBI SAMIA ARDHI KLINIKI YAANZA PWANI

HALMASHAURI ya Manispaa Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeweka kambi ya Samia Ardhi Kliniki ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

Akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa katika kambi hiyo ya siku sita, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Rugambwa Banyika alisema kuwa kliniki hiyo inalenga kutoa ushauri wa kisheria kuhusu masuala ya ardhi.

Banyika alisema kuwa shughuli nyingine zitakuwa ni kufanya makadirio ya pango la ardhi, kuandaa nyaraka za umiliki, kujibu changamoto za upimaji, urasimishaji, upangaji miji na michoro pamoja na kutoa hati za umiliki.

"Wananchi wote wanakaribishwa ili kupata huduma zote zihusiananazo na masuala ya ardhi ambapo huduma zimesogezwa ili kila mwananchi apate fursa katika kipindi hichi kuanzia Machi 2 hadi 7 kuelekea kilele cha siku ya Wanawake Duniani Machi 8,"alisema Banyika. 

Alisema kuwa kambi hiyo maalum ina lengo la kushughulikia changamoto mbalimbali za ardhi kwa wananchi hususan wanawake na wasichana katika masuala yanayohusiana na ardhi.

Baadhi ya wananchi Mariam Juma na Ahmed Abdala wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna wanavyohudumiwa na wataalamu wa ardhi kwani wanatoa elimu ya kujitosheleza.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kimkoa kinatarajiwa kufanyika Machi 8 2026 katika Uwanja wa Ujamaa Kata ya Umwe Tarafa ya Ikwiriri Halmashauri ya Mji wa Rufiji ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

No comments:

Post a Comment