MKOA wa Pwani umesema utashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha inakusanya mapato ili kuinua uchumi kupitia uwekezaji wa viwanda kumuunga Mkono Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
Hayo yelisemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Pili Mnyema wakati wa sherehe za kutimiza miaka 30 ya TRA kimkoa ambapo walushuhudia moja kwa moja maadhimisho hayo Kitaifa ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Dk Samia.
Mnyema alisema kuwa kama Rais alivyotaka TRA kufanya vizuri ili akistaafu Mamlaka hiyo iwe kwenye hali nzuri ndiyo itakuwa furaha yake.
"Tutamuunga mkono Rais kwa kushirikiana na TRA kuhakikisha walipa kodi wanalipa kodi pasipo kukwepa kodi ili kuinua uchumi hasa ikizingatiwa Pwani ni mkoa wa kimkakati kwa kuwa na viwanda vingi,"alisema Mnyema.
Alisema kuwa ukusanyaji mzuri unaofanyika unatokana ushirikiano uliopo baina ya mamlaka na walipa kodi ambapo hicho ni kiashiria cha ukuaji wa uchumi.
"Pia ukusanyaji utaendana na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050 ambayo ndo inaanza kazi kuanzia sasa na hapa tunashirikiana na sekta binafsi katika kuchangia uchumi,"alisema Mnyema.
Aidha alisema kuwa Mkoa utasimamia kuhakikisha malengo ya nchi yanatimia kwa kuwa na uwezo wa kukusanya mapato kwa walipa kodi kulipa kwa hiyari ikiwa ni maono ya Rais.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Salim Makame alisema kuwa Mamlaka imejipanga kuhakikisha wale wote wanastahiki kulipa wanalipa kwa hiyari.
Makame alisema kuwa wameyapokea maagizo yote yaliyotolewa na Rais ya namna ya kuboresha ukusanyaji wa Mapato pia kutumia mifumo ya teknolojia.


