Saturday, August 1, 2026

HALMASHAURI YA MANISPAA KIBAHA YAZINDUA MAGARI MRADI WA (TACTIC)

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imezindua magari mawili yatakayotumika kwenye mradi wa ujenzi wa barabara za lami kwenye kupitia mradi wa uboreshaji miundombinu ya Miji na Vijiji (TACTIC) wenye thamani ya shilingi bilioni 19.8

Akindua magari hayo ambayo yatatumika kwenye mradi huo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo alisema magari hayo yatawezesha utekelezaji mradi kuwa rahisi.

Mawazo alisema kuwa magari hayo ni moja ya makubaliano mkataba wa mradi huo na yakimaliza kutumika yanarudi Halmashauri kwa ajili ya shughuli zingine za kutoa huduma kwa wananchi kupitia wataalamu.

"Mradi huu unaenda kuleta mabadiliko chanya na uboreshaji wa miundo mbinu mbalimbali ya Manispaa ya Kibaha na kuwa na mwonekano mzuri na kuleta urahisi wa usafiri na usafirishaji,"alisema Mawazo.

Alisema kuwa katika miradi hiyo ya Tactic wanakwenda kuitekeleza kwa ubora zaidi na Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inaenda kuwa ya kwanza na mfano kwa Halmashauri zingine katika utekelezaji na usimamizi wa miradi hii nchini.

"Wananchi wa Kibaha wanapaswa kujivunia na kutangaza maendeleo yanayofanywa na serikali hii kwani Manispaa ya Kibaha ina neemeka na dira ya Rais na mmeona maendeleo yanavyokuja kwa kasi na tutakuwa Halmashauri ya mfano kwa kila kitu,"alisema Mawazo.

Akisoma taarifa ya mradi huo Ofisa Utumishi  Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuleta miradi yenye fedha nyingi na usimamizi mzuri wa viongozi wa Wilaya na Mkoa kwa utekelezaji wa Ilani kwa maslahi ya Manispaa ya Kibaha.

Mlela alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa kwa usimamizi mzuri wa masuala mbalimbali ya mapato usimamizi wa miradi pamoja na tija katika utendaji wa Halmashauri.

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imepokea magari hayo mawili kutoka kwenye Mkataba wa mradi wa Tactic ambapo yatatumika katika mradi wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 4.8 Tughe-Anglikana barabara ya Picha ya Ndege - Lulanzi na soko la Loliondo Mnarani.

MADARASA JANJA KUPUNGUZA CHANGAMOTO UPUNGUFU WA WALIMU NCHINI

MEYA wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Nicas Mawazo amezindua Darasa Janja (Live Teaching) Shule ya Sekondari Bundikani na kuiomba Serikali kuanzisha madarasa hayo kote nchini ili kukabiliana na upungufu wa walimu

Mawazo alitoa ombi hilo wakati akizindua darasa hilo shuleni hapo ambapo shule hiyo ni Sekondari ya Kata ya Maili Moja Wilayani Kibaha na kuwa darasa janja yatasaidia kuwafanya wanafunzi kuwa na ari ya kusoma.

Amesema kuwa mwalimu mmoja anayefundisha kupitia darasa janja moja anaweza kufundisha shule zote ambazo zitakuwa zimeunganishwa kwenye mfumo huo wa darasa la aina hiyo kote nchini kwa wakati mmoja.

"Mfumo huu wa darasa janja ni mzuri kwa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu kwani mwalimu mmoja anauwezo kufundisha shule zote ambazo zimeunganishwa kwenye mfumo huo,"amesema Nicas.

Aidha amesema kuwa pia mbali ya kufundisha wakati mmoja pia yale aliyofundisha mwalimu huyo yanaweza kurekodiwa na kuwafundisha wanafunzi wengine kwa ubora ule ule.

"Jambo zuri ni kuwa walimu wote wanaofundisha kupitia madarasa janja wote ni wale wenye umahiri wa kufundisha hivyo watawajengea wanafunzi uwezo mkubwa wa kujifunza na kupata ujuzi,"amesema Mawazo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mrisho Mlela amesema kuwa wataendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa janja kwenye shule za sekondari.

Mlela amesema kuwa wameendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule tatu za mfumo wa Kiingereza na shule hizo zote zimejengwa kutokana na fedha za mapato ya ndani na kutengeneza madawati viti na meza 4,000 kwa shule za msingi na sekondari.

Naye Mkuu wa Shule ya Bundikani Bernard Muyenjwa amesema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia darasa hilo janja kwani litarahisisha katika ufundishaji na kupunguza changamoto ya upungufu wa walimu.

Muyenjwa amesema kuwa kuanzishwa kwa darasa janja hilo shuleni kwao kutasaidia walimu kufundisha bila ya kuchoka wala kutumia nguvu kubwa na kuwapa wanafunzi umahiri na kujua namna ya kutumia teknolojia.

mwisho