Monday, August 10, 2026

WANNE WAFA 46 WAJERUHIWA AJALINI

WATU wanne wamefariki dunia na wengine 46 kujeruhiwa baada ya basi dogo walilokuwa wakisafiria kutoka Vikumburu Kisarawe kwenda Dar es Salaam kupinduka.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Salim Morcase ilisema kuwa basi hilo liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.

Morcase alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Agosti  9 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni huko eneo la kona ya Kinyanyiko katika barabara ya Pugu Kisarawe Wilaya ya Kisarawe.

"Gari lenye namba za usajili T 177 DBV aina ya Fuso likitokea Vikumburu kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na Salehe Mtumwa (35) na Mkazi wa Chanika Dar es Salaam liliacha barabara na kupinduka kisha kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi kwa watu 46,"alisema Morcase.

Alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi ambapo dereva alishindwa kulimudu gari kwenye mteremko mkali hivyo kupelekea gari hilo kupinduka.

Aliwataja waliofariki kuwa ni dereva wa gari hilo Salehe Mtumwa (35) na Mkazi wa Chanika Dar es Salaam,  Mwika Gwesele (38) Mkazi wa Dar es Salaam, Fatuma Momba Mkazi wa Buguruni Dar es Salaam na Sivijui Samatha (40) Mkazi wa Dar es Salaam.

Aliwataja majeruhi wanaopatiwa matibabu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni Hamis Mtitu (55) Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, Farida Hassan (28) Mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam, Husna Bakari (26) Mkazi wa Buza Dar es Salaam, Radhia Sultan (36)Mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Neema Hassan (42) Mkazi wa Temeke, Dar es Salaam.

Majeruhi wengine ni Pilli Kondo (40) Mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Salama Ramadhan (40)Mkazi wa Kigogo Dar es Salaam, Salumu Rajabu (56) Mkazi wa Mbande Dar es Salaam, Pilli Habibu (28) Mkazi wa Majohe Dar es Salaam, Amina Ramadhan (64) Mkazi wa Boga Wilaya ya Kisarawe.

"Majeruhi wengine saba wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe ambapo kati yao wanaume ni watatu na wanawake ni wanne huku majeruhi wengine 29 wamepatiwa matibabu katika Hospitali hiyo ya Kisarawe na kuruhusiwa," alisema Morcase.

Aidha alisema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawataka madereva wote wa vyombo vya moto kuzingatia sheria ya usalama barabarani pamoja na kanuni zake ili kuepusha ajali zinazosababishwa na uzembe. 

"Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa madereva watakaosababisha ajali kwa uzembe au kutokuzingatia sheria za usalama barabarani na kanuni zake,"alisema Morcase.

No comments:

Post a Comment