MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni moja kwa Shina la Wakereketwa wa Umoja wa Bodaboda Nida (UWB) Kata ya Tangini Wilayani Kibaha.
Alikabidhi kiasi hicho cha fedha wakati alipokuwa akitembelea miradi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya hiyo kwenye Baraza la kawaida la Kata.
Koka amesema kuwa wao kama wabunge wamekuwa wakiwatetea madereva wa bodaboda bungeni ili kuhakikisha wanarasimishwa na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.
"Hata Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha madereva wa bodaboda ili nao wanufaike na asilimia 10 zinazotokana na mapato ya ndani,"amesema Koka.
Amewataka madereva wa bodaboda kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia taratibu ili waweze kufanikiwa na kuepukana na utendaji kazi ambao haifuati sheria.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tangini Antony Millao amesema kuwa amekuwa akikisaidia kikundi hicho ili kuhakikisha kinafuata taratibu.
Millao amesema kuwa moja ya changamoto waliyonayo ni ukosefu wa leseni lakini wanaendelea kuitatua changamoto hiyo kwa kuwatafutia madarasa ya kupata elimu ya udereva.
Naye Katibu wa UVCCM Kata ya Tangini Lazaro Benjamin amesema kuwa wameanzisha mradi wa kuosha magari ambapo wanahitaji kupata vifaa kwa ajili ya mradi huo.
Benjamin amesema lengo la kusnzisha mradi huo ni kujiongezea kipato badala ya kuomba fedha kutoka kwa wadau kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.

No comments:
Post a Comment