Thursday, August 20, 2026

RAIS DK SAMIA SULUHU HASSAN KUZINDUA MRADI BWAWA LA KUFUA UMEME LA MWALIMU JULIUS NYERERE RUFIJI

KUELEKEA uzinduzi wa mradi wa Bwawa la kufua umeme la la Mwalimu Julius Nyerere Rufiji unaotarajiwa kufanywa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan Agosti 22 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amebainisha mafanikio yaliyotokana na mradi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha kuhusu uzinduzi huo alisema kuwa tukio hilo ni la kihistoria na unatimiza ndoto za Watanzania.

Kunenge alitaja baadhi ya faida ya mradi huo kuwa ni pamoja na Mkoa hadi kufika Julai kupata megawati 356 kutoka megawati 118 za umeme mwaka 2022.

"Kwa sasa umeme umeingizwa kwenye gridi ya umeme ya Taifa na kuna kituo cha kupooza umeme kilichopo Chalinze ambapo kuna kv 400 zinazopelekwa Mkoani Dodoma,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa vituo vingine vya vitakavyojengwa ni Kwala, Zegereni na Zinga na mradi huo mbali ya kuhudumia wananchi pia ziada itauzwa nje ya nchi ambapo kwa sasa umeme ni wa uhakika.

"Uwekezaji wa viwanda vikubwa na vya kati umeongezeka kwa viwanda 307 ambapo imetokana na kuwa na uhakika wa nishati ya umeme na sasa kuna mpango wa kuleta gesi kutoka Kinyerezi kwenda Chalinze,"alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa kwa sasa vijiji vyote vya Mkoa wa Pwani vina umeme ukiondoa vijiji nane vilivyopo Visiwani ambavyo vinatumia umeme wa jua.

"Pia kwa sasa upembuzi yakinifu unafanyika eneo la Mloka ambapo kutajengwa bwawa la maji safi ambapo mbali ya Mkoa wa Pwani pia mikoa ya Morogoro na Lindi itanufaika na mradi huo utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 1.5 lakini kwa kuanzia utazalisha lita 750,000 kwa siku,"alisema Kunenge.

Aliongeza kuwa upembuzi unaendelea kwa ajili ya kuwa na mabwawa kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji eneo la Mkongo na Kibiti kwa maji yatakayokuwa yanatoka kwenye mradi huo na kuondoa mafuriko ambayo hutokea kipindi cha mvua.

"Hatimaye Tanzania imetimiza ndoto ya Nyerere ya kujitosheleza kwa umeme ambapo bwawa linazalisha umeme megawati 2,115 na uzinduzi ni historia na tunatarajia wananchi kujitokeza kwa wingi na wageni kutoka nje ya nchi,"alisema Kunenge.

Mradi huo una thamani ya shilingi trilioni saba na ulianza awamu ya tano ya Hayati Dk John Pombe Magufuli na Rais Dk Samia Suluhu Hassan aliukuta ukiwa asilimia 35 na kuukamilisha na kutimiza ndoto za Watanzania.

No comments:

Post a Comment