Friday, August 14, 2026

WAKUFUNZI WA VYAMA SITA RAFIKI WANOLEWA

VYAMA Sita Rafiki vya Ukombozi Kusini mwa Afrika vimetakiwa kuendeleza ushirikiano ulioachwa na waasisi wa mataifa hayo ili kuleta maendeleo kwa wananchi.

Hayo yamesemwa kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS) Kwa Mfipa Kibaha na Katibu Mkuu wa Chama cha SWAPO na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Shule hiyo Sophia Shaningwa wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Programu hiyo.

Shaningwa amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia wakufunzi hao kuwajengea uwezo viongozi wa vyama hivyo tawala kwani wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Aggrey Mwanri ameipongeza shule hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wakufunzi kwani yatasaidia kuleta maendeleo na kukuza uchumi.

Mwanri amesema kuwa huo ni uwekezaji mzuri kwa viongozi ili kupata mbinu mbalimbali ikiwemo za mawsiliano na kuhudumia kwa usawa.

Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Kitaaluma na Wanafunzi wa Shule hiyo Profesa Ana Nhampule akielezea kuhusu mafunzo hayo amesema kuwa Shule inavihudumia vyama sita rafiki na kundi pana la viongozi kupitia programu zinazohusiana na vyama, programu maalum kwa ajili ya wizara, taasisi za umma, biashara, na mashirika mengine, pamoja na programu huru kwa viongozi chipukizi na wale waliothibitika. 

Nhampule amesema kuwa Mkakati wao unajumuisha uongozi wa vijana EYOLE uongozi wa wanawake kupitia SIWOLEMA, usimamizi wa mashirika ya umma kupitia SLM-PESA na programu za mkakati, utawala, maadili, majadiliano, mawasiliano, mabadiliko ya kiuchumi, maslahi ya taifa, na utendaji wa kitaasisi. 

"Katika mzunguko wa Mpango Mkakati wa 2023-2025 MJNLS ilitekeleza programu 93 na kufundisha au kuhitimu washiriki 14,735 inakua kama taasisi ya maarifa ,"amesema Nhampule.

Aidha amesema kuwa ajenda yao ya Utafiti 2025-2035 inaungwa mkono na miundo ya Baraza la Mawazo, Jarida la Uongozi na maktaba inayozidi kukua na ushirikiano wa kieneo wa utafiti.

Vyama hivyo rafiki vinavyoshiriki mafunzo hayo ya siku 45 ni CCM ina 10, ANC tisa, FRELIMO watano , SWAPO watatu, na ZANU-PF 10 ambapo wajumbe wa MPLA hawakuweza kufika kutokana na shughuli za sasa na za dharura za chama chao.

mwisho. 

No comments:

Post a Comment