Thursday, October 1, 2026

LAZARO BIYA ACHAGULIWA MWENYEKITI WA CCM KATA YA TANGINI

LAZARO Biya amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tangini Wilaya ya Kibaha Mjini kwenye uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo.

Uchaguzi huo umefanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti Antony Millao ambaye alichaguliwa kuwa Diwani wa Kata hiyo kwenye uchaguzi Mkuu uliopita.

Msimamizi wa uchaguzi huo Frank Msimbe alimtangaza Biya kupata kura 93 huku Mfalme Kalanguti akipata kura 37 kati ya kura 131 zilizopigwa ambapo hakuna kura iliyoharibika.

Akizungumza mara baada ya kushika nafasi hiyo Biya amesema kuwa anawashukuru wajumbe kwa kumpigia kura na kumwamini kumpa nafasi hiyo na kuahidi kuwatumikia wanaCCM na wananchi wa Kata hiyo.

Biya amesema kuwa atakuwa kiongozi wa wanachama wote siyo wa kundi fulani na maamuzi atakayoyatoa ni yale yatakayotokana na vikao siyo mawazo yake.

"Moja ya vipaumbele vyangu itakuwa ni kufuatilia kuhusiana na kitega uchumi cha chama ikiwemo sehemu ya vinywaji mgahawa ili vianze kazi kwani miradi hiyo iko hatua ya mwisho kukamilika,"amesema Biya.

Amesema atahakikisha anawaunganisha wanachama ili wawe kitu kimoja na kusimamia suala zima la mendeleo kwani iko kwenye ilani ya chama.

Naye Kalanguti amekubaliana na matokeo hayo kwani uchaguzi ni mchakato kikubwa ni kuendelea kushirikiana ili chama kiweze kuwaletea maendeleo wananchi.