Tuesday, May 5, 2026

VIJANA WATAKA MFUMO UKOPAJI UBORESHWE KUVUTIA VIJANA

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kibaha Mjini umeishauri Wizara ya Maendeleo ya Vijana kuangalia upya mfumo wanamna ya kuwapata vijana kukopa ili wengi waweze kunufaika.

Akizungumza ofisini kwake Katibu wa (UVCCM) Kata ya Tangini Lazaro Benjamin alisema kuwa Wizara inapaswa kuweka mfumo rafiki na kuweka masharti nafuu.

Benjamin alisema kuwa kuweka masharti magumu kunakwamisha vijana wengi kupata fursa ya kufikia mikopo hiyo inayowalenga vijana.

"Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa wanapokosa mitaji wanakosa fursa ya kujiajiri na matokeo yake ni kuongezeka kwa ukosefu wa ajira umasikini na hata kukata tamaa,"alisema Benjamin.

Alisema kuwa kuna umuhimu sasa wa kuongeza bajeti ya mikopo ya vijana ili iwafikie wengi zaidi pia kutoa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha ili mikopo itumike kwa ufanisi.

"Lengo liwe ni kuwafikia vijana wengi zaidi iwezekanavyo kwani maendeleo ya Taifa letu yanategemea uwezeshaji wa vijana wake na wafanye maboresho ili kuhakikisha uwiano unazingatiwa,"alisema Benjamin.

Aidha alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi kwani hiyo ni hatua kubwa na ya kupongezwa na inaonesha dhamira ya kweli ya serikali katika kuinua vijana wa Taifa la Tanzania.

"Wizara ifanye utafiti kwani takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya vijana 30,384 waliomba mikopo hii lakini vijana waliokidhi vigezo vya kukopeshwa ni 1,961tu,"alisema Benjamin.

Aliongeza kuwa idadi kubwa sana ya vijana zaidi ya asilimia 90 hawakupata fursa hiyo utafiti ufanyike ili kujua ni kwa nini idadi hiyo kutokidhi vigezo na kama bajeti ni ndogo basi iongezwe ili asilimia ya vijana wanaoomba mikopo waweze kuongezeka na kupanua wigo wa ajira kwani wakipata watajiajiri.