Hayo yalisemwa na Katibu wa (UWWM) Mwinjilisti Williama Wami wakati wa uzinduzi wa umoja huo na Mfuko wa umoja ambapo changamoto ya usafiri ni kubwa kwani kuna basi moja tu linalofanya safari zake kati ya Mkombozi na Mbezi Jijini Dar es Salaam.
Wami alisema Mtaa huo umepakana na Wilaya ya Ubungo ambapo wanapata mahitaji yao eneo la Kibamba Njia Panda Shule kutokana na ukaribu tofauti na Kibaha ambako ni mbali.
"Wakazi huku ni wengi sana lakini tatizo kubwa ni usafiri ambapo kutokana na ubovu wa barabara magari mengi hayawezi kufika kwani kuna basi moja tu ambalo linatoa huduma lakini sisi malengo yetu ni kununua mabasi madogo mawili ili kurahisisha usafiri,"alisema Wami
Alisema kuwa kwa sasa wanatumia usafiri wa pikipiki ili kufika majumbani au kutoka kwenda kwenye shughuli zao za kila siku kujiletea kipato lakini usafiri huo ni gharama kubwa sana.
"Kupitia umoja wetu tulihamadisha kupatikana kwa basi hilo lakini bado halikidhi mahitaji kwani uhitaji ni mkubwa sana kwani uwezo wa baadhi ya watu kupanda pikipiki kwao ni mzigo mkubwa lakini kupitia daladala gharama inakuwa nafuu,"alisema Wami.
Aidha alisema kuwa malengo yao mengine ni kujenga ukumbi mkubwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo mikutano na sherehe utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 500 ambapo kwa sasa huwabidi kufanya shughuli hizo nje ya mtaa huo pia kuanzisha Chama Akiba na Mikopo ili kukopeshana kwa riba nafuu.
"Vitu tulivyofanya ni kuvuta maji na kujenga vyoo vya kisasa kwenye soko jipya na tunatarajia hapo kuwa na stendi tunaishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kutuanzishia soko tunaomba watupe kibali ili watu waanze kufanya biashara,"alisema Wami.
Aliongeza kuwa miradi hiyo mbali ya kutoa huduma itakuwa ni vyanzo vya mapato ya umoja kwani lengo ni kuleta maendeleo ya Mtaa na kwa mwananchi mmoja mmoja pia ni kusaidiana katika shida na raha na kauli mbiu ni Baba kichwa cha Familia.
Umoja huo ulianzishwa mwaka jana na una wanachama 265 huku wanachama hai ni 205 hadi sasa wana kiasi cha shilingi milioni 10 benki ambapo kila mwezi mwanachama huchanga shilingi 5,000.

No comments:
Post a Comment