WATENDAJI wa Kata Mkoani Pwani wametakiwa kumsadia Rais kwenye suala la ukusanyaji wa mapato ili yaweze kuleta maendeleo kwa wananchi ili kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa Kikao kazi cha watendaji wa Kata wa Mkoa huo kilichofanyika Kibaha.
Kunenge alisema kuwa Mkoa kwa sasa unafanya vizuri kwenye suala la ukusanyaji wa mapato hapa nchini kutokana na kuweka mazingira mazuri kwa kwenye maeneo ya vyanzo vya mapato.
"Nyie ni watu muhimu sana na serikali ingependa kuona mnaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo inataka pato la mtu lifikie dola 7,000 kwa mwaka na la nchi trilioni 1 hadi ifikapo mwaka 2050,"alisema Kunenge.
Alisema wakati anafika kwenye Mkoa huo ulikuwa ni moja ya mikoa iliyokuwa chini kimapato ikiwa ni Mkoa wa 23 lakini kwa sasa umeweza kuinuka kimapato.
"Mnapofanya shughuli zenu mhakikishe mnazingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa inaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi ili iendeshe uchumi kuzalisha ajira kuongeza thamani ya mazao na kuuza nje ya nchi,"alisema Kunenge.
Alisema kuwa sekta binafsi ni ya kimageuzi ili kuwe na mabadiliko ambapo asilimia 70 ya maendeleo inatokana na sekta binafsi hivyo lazima kuweka mazingira mazuri hasa ikizingatiwa Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi.
"Watendaji wa kata ni muhimu kwani ni sehemu muhimu ya maendeleo na mabadiliko hivyo hawapaswi kufanya kazi kwa mazoea kwani dunia inabadilika,"alisema Kunenge.
Aidha alisema kuwa wasiamini kwenye kushindwa bali waamini kwenye kushinda kwani wanatakiwa kuongeza thamani na hawapaswi kulala kama anavyofanya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye halali ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Alibainisha kuwa watendaji hao wanapaswa kupunguza kero na rasilimali zinazopatikana zitumike kwa kuzingatia vipaumbele vya eneo husika na waongeze mapato ya ndani ili nchi iweze kujitegemea.
Nao watendaji hao walisema kuwa watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kushirikiana na viongozi wao na wadau ili kufikia malengo hayo yaliyowekwa ili kuleta maendeleo.

No comments:
Post a Comment