MKOA wa Pwani umeongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 87.9 Juni kwa mwaka 2025 na kufikia asilimia 106 Machi mwaka 2026.
Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati wa Kikao kazi cha watendaji wa Kata wa Mkoa huo.
Kunenge amesema kuwa Mkoa unafanya vizuri kwenye suala la ukusanyaji wa mapato hapa nchini kutokana na kuweka mazingira mazuri.
"Nyie ni watu muhimu sana na serikali ingependa kuona mnaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo inataka pato la mtu lifikie dola 7,000 kwa mwaka na la nchi trilioni 1 hadi ifikapo mwaka 2050,"amesema Kunenge.
Amesema wakati anafika kwenye Mkoa huo ulikuwa ni moja ya mikoa iliyokuwa chini kimapato ikiwa ni Mkoa wa 23 lakini kwa sasa umeweza kuinuka kimapato.
"Mnapofanya shughuli zenu mhakikishe mnazingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa inaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi ili iendeshe uchumi kuzalisha ajira kuongeza thamani ya mazao na kuuza nje ya nchi,"amesema Kunenge.
Amesema kuwa sekta binafsi ni ya kimageuzi ili kuwe na mabadiliko ambapo asilimia 70 ya maendeleo inatokana na sekta binafsi hivyo lazima kuweka mazingira mazuri hasa ikizingatiwa Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi.
"Watendaji wa kata ni muhimu kwani ni sehemu muhimu ya maendeleo na mabadiliko hivyo hawapaswi kufanya kazi kwa mazoea kwani dunia inabadilika,"amesema Kunenge.
Aidha amesema kuwa wasiamini kwenye kushindwa bali waamini kwenye kushinda kwani wanatakiwa kuongeza thamani na hawapaswi kulala kama anavyofanya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye halali ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Alibainisha kuwa watendaji hao wanapaswa kupunguza kero na rasilimali zinazopatikana zitumike kwa kuzingatia vipaumbele vya eneo husika na waongeze mapato ya ndani ili nchi iweze kujitegemea.

No comments:
Post a Comment