Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salim Morcase alisema kuwa mara baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.
Morcase alisema kuwa tukio hilo lilitokea Mei 22 mwaka huu huko maeneo ya Tungutungu Mapinga Wilayani Bagamoyo ambapo kati yao ng’ombe 13 ni mali ya Fadhili Ngabilo mkazi wa Kwa Makocho Kata ya Mandela Chalinze
"Mlalamikaji Fadhili Ngabilo aliripoti katika kituo cha Polisi Chalinze kuibiwa jumla ya ng’ombe 18 na mbuzi watano ambapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo(STPU) walianza ufuatiliaji,"alisema Morcase.
Alisema kuwa katika ufuatiliaji ilipofika Mei 22 majira ya saa 3:00 asubuhi walifanikiwa kuwapata ng’ombe 28 wakiwemo ng’ombe 13 kati ya 18 walioibiwa Chalinze wakiwa kwenye zizi la mfanyabiashara mmoja wa nyama.
"Kati ya ng’ombe 15 waliokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa ng’ombe watano walitambulika na ng’ombe wanne mahojiano yanaendelea,"alisema Morcase.
Aidha alisema kuwa mtuhumiwa huyo huwa anachinja ng’ombe wa wizi nyumbani kwake kisha kuuza nyama kwenye bucha yake.
"Hadi sasa jumla ya watuhumiwa wanne wanashikiliwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kuhusiana na tukio hilo,"alisema Morcase.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi kwa kadri operesheni za kudhibiti uhalifu zinavyofanyika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Pwani.

No comments:
Post a Comment