Thursday, May 14, 2026

UMOJA WA WANAUME MKOMBOZI WASAIDIA KUPATIKANA DAMU CHUPA 13



UMOJA wa Wanaume Mkombozi (UWWM) umefanikisha kupatikana kwa damu kiasi cha chupa 13 kwa ajili ya Kituo cha Afya Kata ya Pangani Wilayani Kibaha.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa umoja  kilichopo Mtaa wa Mkombozi Wilayani Kibaha Katibu wa UWWM Mwinjilisti William Wami alisema kuwa lengo ni kuisaidia wagonjwa kwenye kituo hicho.

Wami alisema kuwa umoja huo ulianzishwa kwa ajili ya kuisaidia jamii katika masuala mbalimbali ili kuleta maendeleo kwenye Mtaa huo na Wilaya nzima ya Kibaha.

"Mbali ya kuchangia damu pia tumepanda miti kwenye eneo itakapojengwa Zahanati kwenye Kituo cha Afya cha Kata ya Pangani na Shule ya Msingi Mkombozi lengo likiwa ni kutunza mazingira kwenye maeneo hayo,"alisema Wami.

Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo Diwani wa Kata ya Pangani John Katele ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha alisema kuwa umoja huo umeonyesha moyo wa kibinadamu wa kujitolea ili kunusuru maisha ya wengine.

Katele alisema kuwa damu ni muhimu sana hasa kwa wanawake ambao wanajifungua kwani huhitaji damu nyingi au wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kwenye kituo hicho. 

Katele alisema kuwa jamii inapaswa kujitolea ili kukabiliana na changamoto ya damu kwenye kituo hicho hivyo kupunguza changamoto hiyo kwani damu huhitajika wakati wote.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho Alex Ditopile alisema kuwa anawashukuru wananchi waliojitolea damu kwani tayari wameshaanza kuzalisha mama wajawazito na matumizi ya damu ni makubwa kwani kwa mwezi wanatumia chupa 10.

Ditopile alisema kuwa kwa sasa wana chupa tano na inapotokea wameishiwa damu huchukua Kituo cha Afya cha Lulanzi na kwa sasa wanapokea wagonjwa wengi tangu kituo hicho kilipofunguliwa Desemba 2025.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkombozi Jackson Msaki alisema kuwa kikundi hicho ni kwa ajili ya wanaume wote kwenye Mtaa huo na haubagui mtu yoyote.

Msaki alisema kuwa umoja huo umeweza kuhamasisha kupatika kwa usafiri wa daladala kutokea Mtaa huo hadi Mbezi kujenga choo na kuvuta maji kwenye soko jipya.

Umoja huo ulianzishwa mwaka 2025 kikiwa na wanachama 105 huku kwa sasa kikiwa na wanachama 265 hai wakiwa 205 kikiwa na kauli mbiu ya "Mwanaume Kichwa cha Familia".


No comments:

Post a Comment