Sunday, May 24, 2026

MTAA WA MWENDAPOLE B MBIONI KUANZA ULINZI SHIRIKISH KUKABILI UHALIFUI

WANANCHI wa Mtaa wa Mwendapole B Wilayani Kibaha wamekubaliana kuanza kufanya ulinzi shirikishi ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu ndani ya Mtaa huo..

Akizungumza na wananchi wakati wa kikao cha Mtaa kilichofanyika kwenye ofisi za Mtaa huo Mwenyekiti wa Mtaa Abubakar Matumla alisema kuwa kabla ya kuanza kamati itakaa ili kuangalia namna ya kufanya ulinzi huo.

Matumla alisema tayari wameshapata kibali cha kuwa na ulinzi shirikishi na kinachofuata ni kupanga namna ya kufanya zoezi hilo na namna wananchi watakavyo changia watu watakaokuwa wakilinda.

"Tunamshukuru Mkuu wa Wilaya tayari katoa kibali cha Mtaa kuwa na ulinzi shirikishi ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa vikijitokeza nyakati tofauti tofauti,"alisema Matumla.

Alisema kuwa watakaa na kamati ya Mtaa wiki hii ili kupanga utaratibu mzuri wa kuanza zoezi hilo na kiwango cha kila kaya kuchangia ili kuwalipa walinzi hasa ikizingatiwa michongo ya ulinzi shirikishi ni hayari.

Aidha alisema kuwa wenye nyumba nao wsnapaswa kuwa makini kwa kuwa na taarifa za kutosha za wapangaji wao kwani baadhi yao wanaweza kuwa wanajihusisha na uhalifu.

Naye Diwani wa Kata ya Kibaha Omary Bulla alisema kuwa ulinzi shirikishi ni muhimu sana kwani baadhi ya vijana ambao siyo waaminifu wamekuwa wakiiba vitu kwenye nyumba au kukaba watu.

Bulla alisema kuwa ili kufanikiwa wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu kwa kutoa michango ili iwezeshe walinzi waweze kufanya kazi zao bila ya vikwazo na kukabili uhalifu ndani ya Mtaa huo.

Kwa upande wake mmoja wa wananchi wa Mtaa huo Dago Mwombeki alisema kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakiwapora watu wanaokuwa wanakwenda kazini alfajiri au wanapokuwa wanatoka kazini.

Mwombeki alisema kuwa ulinzi shirikishi utasaidia kukabili changamoto hiyo ya uhalifu ndani ya Mtaa kwani wanasababisha watu wasiishi kwa amani na kurudisha nyuma maendeleo ya watu.

No comments:

Post a Comment