Sunday, November 1, 2026

WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA MSAADA WA KISHERIA WA MAMA SAMIA

WANANCHI wenye changamoto za kisheria Mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza kupata huduma kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid).

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa  Mkoa huo Richard Kayombo baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya kampeni hiyo yaliyopo stendi ya zamani ya Maili Moja Manispaa ya Kibaha.

Kayombo amesema kuwa Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa yenye migogoro mingi ya ardhi na baadhi imekuwa ikichangiwa na kasoro katika hatua za awali za mauziano.

"Wananchi wanapaswa kujitokeza ili kupata elimu ushauri na miongozo ya kisheria itakayowasaidia kutatua changamoto zao hivyo wananchi wanapaswa kupata elimu ili kujiepusha na migogoro hiyo,"amesema Kayombo.

Amesema kuwa mbali ya kutatuliwa migogoro ya ardhi pia migogoro mingine ni kama vile ya ndoa mirathi matunzo ya watoto vitendo vya ukatili ajira na madai.

Kwa upande wake Mratibu wa kampeni hiyo Wakili Innocent Magesa amesema kuwa mwamko wa wananchi katika siku tatu za awali umekuwa mzuri na wataendelea kuongezeka.

Magesa alisema kuwa awamu ya pili ya kampeni hiyo inatekelezwa kwa siku 10 kuanzia Oktoba 28 hadi Novemba 7 mwaka huu na bado wananchi wana siku saba za kunufaika na huduma hizo.

Naye Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani Aneth Mwakatobe amesema kuwa moja ya mashauri yanayopelekwa ofisini kwao ni masuala ya ardhi.

Mwakatobe amesema kuwa katika kuhakikisha elimu juu ya kupambana na vitendo vya rushwa wamekuwa wakiitoa kwenye maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja kwenye Kata ndani ya jamii.