Friday, July 3, 2026

Mpya







MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amemshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuinua vipaji vya wanamichezo vijana ili kuwa tegemeo kwa Taifa.

Kunenge ameyasema hayo wakati akizindua michezo ya riadha Kitaifa kwenye uwanja wa Filbert Bayi Mkuza Wilayani Kibaha.

Amesema kuwa Rais ameweka mazingira mazuri kwa wanamichezo nchini ambapo kwa sasa nchi inafanya vizuri kwenye michezo mbalimbali ikiwemo riadha.

"Nawapongeza Shirikisho la Riadha Tanzania kwa kuweka misingi mizuri kwa vijana wadogo ambao wameonyesha umahiri wa kukimbia licha ya kuwa na umri mdogo huu ndiyo uwekezaji mzuri kwenye vipaji,"amesema Kunenge.

Aidha amesema kuwa riadha ni mchezo ambao hupambani na mpinzani wako bali unapambana na rekodi hata ukishinda kama hujafikia rekodi nzuri bado hujapata mafanikio.

"Nimefurahi nimewaona manguli wa riadha nchi kama vile Steven Akwari, Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Seleman Nyambui hawa waliiletea nchi sifa kubwa huko duniani vijana wanapaswa kuwaiga ili nao wafanye vyema,"alisema Kunenge.

Amebainisha kuwa Mkoa wa Pwani uko kwenye mipango mbalimbali ya kujenga viwanja ambavyo vitakuwa na ubora ili kupata wanamichezo wazuri wa baadaye.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya ufundi wa Shirikisho la Riadha Tanzania Alfredo Shahanga amesema kuwa wanajivunia kwa wanariadha wake kufanya vizuri akiwemo Alfonce Simbu kwa kushinda medali ya dhahabu kwenye mbio za marathoni za Dunia za Tokyo.

Shahanga amesema kuwa changamoto kubwa ni upungufu wa fedha viwanja vizuri vyenye vifaa vya kisasa na uwekezaji kwa vijana hata hivyo wanashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha changamoto hizo zinapungua na mchezo unachezwa.

Naye katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Pwani Elisha Daniel amesema kuwa mashindano hayo yameanza vyema kwani walifanya maandalizi vizuri na matarajio mwaka huu mafanikio yatakuwa makubwa.

Daniel akizungumzia juu ya timu ya mkoa huo amesema kuwa maandalizi ya timu yako vizuri na wanategemea kufanya vizuri kwani vijana wameandaliwa vizuri na walimu wao lengo ni kuupambania mkoa.

mwisho.

No comments:

Post a Comment