Monday, July 27, 2026

HALMASHAURI MANISPAA YA KIBAHA YAPONGEZWA UKUSANYAJI MAPATO NA UTOAJI MIKOPO KWA VIKUNDI

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Fadhili Maganya ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kuweza kufanikisha ukusanyaji wa mapato.

Maganya ameyasema hayo kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere wakati akizungumza na viongozi wa Jumuiya hiyo wanaccm na uongozi wa Halmashauri wakati wa ziara yake Mkoani Pwani.

Amesema kuwa Halmashauri hiyo imeonyesha jinsi gani inavyopambana katika ukusanyaji wa mapato ambayo yanasaidia katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

"Tunaipongeza Halmashauri kwa jitihada zake za ukusanyaji wa mapato na kuifanya kuwa moja ya Halmashauri zinazofanya vizuri nchini kwenye siala la ukusanyaji wa mapato,"amesema Maganya.

Aidha ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kuvipatia mikopo ya asilimia 10 vikundi vya wajasiriamali kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.

"Kama mmeweza kutoa mikopo na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukopa fedha hizo mnafanya jambo zuri ndivyo serikali inavyotaka wananchi wakopeshwe ili wafanye shughuli zao za kiuchumi,"amesema Maganya.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa amesema kuwa mwaka 2024/2025 walitoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 kwa vikundi 400 vyenye watu zaidi ya 3,000.

Shemwelekwa amesema kuwa changamoto iliyopo ni baadhi ya vikundi kutokuwa na sifa za kukopa lakini fedha zipo kwa vile vinavyokidhi vigezo vinakopeshwa.

Alisema kuwa baada ya mikopo kurejeshwa kulikuwa na madeni yaliyofikia kiasi cha shilingi bilioni 1.2 lakini wamefanya jitihada ya kufanikisha kurejesha na madeni yaliyobakia ni milioni 300.

No comments:

Post a Comment