Wednesday, July 8, 2026

DKT. NICAS MAWAZO AKUTANA NA BALOZI KAIRUKI NCHINI UINGEREZA, WAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI KIBAHA

London, Uingereza | Julai 8, 2026
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo ambaye yupo nchini Uingereza katika ziara nchini humo, leo Julai 8, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Balozi Kairuki.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kairuki amepongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha diplomasia ya uchumi, kuvutia uwekezaji na kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya taifa.

Aidha, Balozi Kairuki ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa mafanikio yake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato ya ndani, akieleza kuwa halmashauri hiyo imeendelea kuwa miongoni mwa halmashauri zinazofanya vizuri nchini.

Mazungumzo kati ya viongozi hao yamejikita katika kutafuta fursa za ushirikiano wa kiuchumi kwa Manispaa ya Kibaha, ikiwemo namna ya kuvutia wahisani, wawekezaji na wadau wa maendeleo kutoka Uingereza ili kuwekeza katika sekta mbalimbali zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya manispaa hiyo.

Dkt. Mawazo amesema kuwa mazungumzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuitangaza Manispaa ya Kibaha kimataifa na kufungua milango ya ushirikiano itakayochochea uwekezaji, ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment