Sunday, July 19, 2026

WANANCHI MTAA WA MACHINJIONI WAJITOLEA KUFUNGUA BARABARA

MTAA wa Machinjioni umefungua barabara ya kuelekea Shule ya Msingi Mamlaka na kurahisisha watumiaji kupita kwa urahisi wakiwemo wanafunzi kwenda Shuleni na magari ya kutoa huduma inapotokea dharura kama vile moto.

Barabara  hiyo ilijifunga wakati wa ujenzi wa barabara ya lami ya kutoka Tamco-Mapinga kuelekea Bagamoyo hivyo kusababisha watumiaji wakiwemo  wanafunzi kuzunguka umbali mrefu ili kwenda shule na kwenye makazi hasa wanaotumia usafiri wa magari na pikipiki.

Akizungumza wakati wa zoezi la kujitolea kufungua barabara hiyo ambayo miaka ya nyuma ilikuwa ikipitika Mwenyekiti wa Mtaa wa Machinjioni Kata ya Tangini Wilaya ya Kibaha Aidan Mchiwa alisema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa eneo hilo.

Mchiwa alisema kuwa barabara hiyo ni muhimu hasa pale endapo ikitokea dharura kama vile moto au wagonjwa ilikuwa ikiwalazimu kuzunguka mbali hasa kwa matumizi ya vyombo vya moto ikiwemo magari na pikipiki.

"Tulikaa na wananchi na kukubaliana kuchanga kiasi cha shilingi 16,000 kila Kaya ili kufanikisha ufunguaji wa barabara hiyo na wananchi waliridhia na zoezi kuanza ambapo pia tuliwasiliana na Dawasa kwani kuna bomba linapita hapo hivyo walitoa wataalamu wao na kutuelekeza namna na kuchimba ili tusiharibu bomba hilo la maji,"alisema Mchiwa.

Emanuel Sabath alisema kuwa wanaushukuru uongozi wa Mtaa kwa kuwafungulia barabara hiyo hivyo kuwarahisishia na kuwaondolea usumbufu kuzungukia mbali na kupita kwenye eneo la mtu.

Sabath alisema kufunguka barabara hiyo kutarahisisha wananchi kupata huduma ikiwa ni pamoja na inapotokea mgonjwa anataka kupelekwa Hospitali wakiwemo wanawake wajawazito na hata gari la zimamoto kupita kwani kulishawahi kutokea moto lakini gari hilo likashindwa kupita.

Alisema kuwa hata wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Mamlaka hasa wanaotoka maeneo ya Kilimahewa ambapo iliwabidi wazunguke kupita sehemu nyingine ambapo huwabidi kuzunguka hivyo kuchelewa kufika shuleni.

No comments:

Post a Comment