Thursday, March 26, 2026

PROGRAM YA MALEZI MAKUZI NA MAENDELEO YA AWALI YA MTOTO YAPATA MAFANIKIO






PROGRAM ya Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto imeleta manufaa makubwa kwa kuanzishwa kadi ya alama kwa watoto inayorahisisha ufuatiliaji.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa Shirika lisilo kuwa la Kiserikali la Anjita Child Development Foundation Janeth Malela wakati wa kikao cha wadau wa Program hiyo Mkoa wa Pwani.

Malela amesema kuwa kuanzishwa kwa kadi hiyo kwa watoto ni mafanikio makubwa ya Program hiyo katika kuhakikisha ustawi wa watoto katika makuzi yake.

Amesema kuwa kikao hicho kiliweza kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya uchechemuzi wa umuhimu wa kuwekeza kwenye Program hiyo na kusaidia serikali kutekeleza Program za malezi.

"Kuendelea kushirikiana na wadau wa nje katika kuwekeza katika malezi kuhamasisha jamii na serikali katika kuanzisha vituo vya kulea watoto wadogo mchana vya jamii,"amesema Malela.

Msajili wa mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali Elia Kabora amesema kuwa uwekezaji kwa watoto ni moja ya vipaumbele ili kuhakikisha makuzi ya watoto yanazingatia upatikanaji wa huduma muhimu.

Kabora amesema kuwa Programu hiyo inalenga kuimarisha utoaji huduma bora za Afya, Lishe, Malezi yenye Mwitikio, ujifunzaji wa Awali na Ulinzi na Usalama kwa watoto wa miaka 0 hadi 8 na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa sekta mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika yasiyo kuwa ya Kiserikali Kibaha Mjini (KITAN) Dk Rose Mkonyi amesema kuwa jamii kwa kushirikiana wadau wengine wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji muhimu ili waweze kupata huduma muhimu.

Mkonyi amesema kuwa wadau wanapaswa kuungana kufanikisha Program hiyo ili kuweza kufanikisha ukuaji na maendeleo ya mtoto kikamilifu kimwili, kiakili, kukuza lugha, mawasiliano kijamii na kihisia. 

Walengwa wa mradi huo walioshiriki kikao hicho ni pamoja na wazazi, walezi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, viongozi wa dini na wataalam wa ngazi ya serikali.

mwisho.

No comments:

Post a Comment