SHULE ya Sekondari Pangani, Manispaa ya Kibaha imefanya zoezi la kupanda miti zaidi ya 344 katika mazingira ya shule hiyo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhimiza taasisi za elimu kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Zoezi hilo limehusisha wanafunzi, walimu pamoja na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Pangani kwa lengo la kuboresha mazingira ya shule hiyo.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Tatu Mwambala amefafanua miti hiyo ni ya kivuli na mbao ambapo miti 220 imetolewa na kitalu cha Manispaa, miti 110 kutoka Wakala wa Misitu kupitia Shule ya Sekondari Msangani II na miti 14 ya matunda imenunuliwa na shule.
Amesema miti hiyo itasaidia kukuza stadi za utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi pamoja na kuboresha mazingira ya shule.
Diwani wa Kata ya Pangani, John Katele amebainisha zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na mikakati ya kupanda miti milioni 1.5 katika mkoa huo.
Kwa upande wake Ofisa Kilimo wa kata hiyo, Omary Ngulengule ameeleza kuwa, wanafunzi wamepata elimu ya vitendo kuhusu uchimbaji mashimo na upandaji sahihi wa miti ili wawe mabalozi wa utunzaji wa mazingira katika jamii.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Stanley Amos ameeleza elimu waliyoipata itawasaidia kuhamasisha familia na jamii kupanda miti na kutunza mazingira.
No comments:
Post a Comment