Sunday, March 22, 2026

UKUWAWAVI WATOA MISAADA KITUO CHA YATIMA BULOMA


UMOJA wa Kusaidiana Wanajeshi Wastaafu wa Vifaru (UKUWAWAVI) wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwenye Kituo cha Kulea Yatima cha Buloma.
Wametoa misaada hiyo ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Iddi el Fitri na Mfungo wa Kwaresma.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi misaada hiyo Mwenyekiti wa (UKUWAWAVI) SSGT Omari Makore amesema kuwa wameguswa kuwasaidia watoto hao ili nao waweze kufurahi kama walivyo watoto wanaoishi na familia zao.

Makore amesema wanajua kuwa watoto hao wana mahitaji mengi lakini wameona
waanze na kidogo walichojaliwa na hiyo ni sadaka na wataendelea kusaidia pale watakapojaliwa wakati mwingine.

"Tutarudi tena kwani watoto hawa wametuonyesha mapenzi makubwa na huu ni mfano na vikundi na watu mbalimbali nao wajitokeze kuwasaidia watoto hawa,"amesema Makore.

Kwa upande wake Mlezi wa (UKUWAWAVI) Brigedia Jenerali Rajabu Hanti (Mstaafu) amesema kuwa watoto hao ni Taifa la kesho wanahitaji malezi ya watu.

Hanti amesema kuwa watoto hao wanapaswa kupelekewa furaha kwa kuwashika mkono kwa misaada mbalimbali ambayo ni mahitaji yao ya msingi.

Naye Mchungaji Jackson Bukelebe amesema kuwa umoja huo umechukua jukumu la kidini kwani dini bora ni ile inayojali yatima watu wanapaswa kujotolea kuwasaidia watoto hao.

Mwasisi wa kituo hicho Anna Kyando amesema kuwa wanashukuru kwa misaada hiyo kwani wadau ndiyo wamekuwa wakiendesha kituo hicho kwani bila wao peke yake asingeweza.

Kyando amesema kuwa changamoto kubwa ni chakula kwani ndicho kinachohitajika muda wote uzio wa ukufa, vifaa vya shule, ada kwa wanafunzi walioko vyuoni kutoka kituo hicho.

Moja ya watoto wa kituo hicho Yohana Almas amesema kuwa wanashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kufanya vizuri kwenye masomo yao na kuomba watu waendelee kuwasaidia.

Baadhi ya vitu vilivyotolewa ni pamoja na mchele kilo 100, unga wa sembe kilo 50, maharage kilo 50, mafuta lita 20, madaftari 100, juisi katoni 5, maji katoni 10, doti 5 za khanga, sabuni za unga, taulo za kike na biskuti.

No comments:

Post a Comment