MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Hawa Mchafu amesema mhimili wa Mahakama unatakiwa kuangalia uwezekano wa kushughulikia kwa karibu changamoto za Wanawake ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Mchafu ambaue pia ni Mbunge Vitimaalumu Mkoa wa Pwani amesema Serikali inatakiwa kuweka madawati ya jinsia na dawati la msaada wa kisheria katika Halmashauri ili Wanawake wanufaike kwa kupata ushauri wa kisaikolojia utakaosaidia kujikwamua kiuchumi kwa kushirikiana na wenza wao ili kupata kipato kwa ajili ya kujikimu na familia zao.
Ametoa angalizo hilo Machi 6 alipokuwa akihutubia wakazi wa Manispaa ya Kibaha walioshiriki kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambapo Manispaa hiyo ilifanya maadhimisho yake mjini Mailimoja.
Katika hotuba yake Mchafu amebainisha kwamba dawati la jinsia Polisi ambalo lina kazi ya kusikiliza na kutoa ushauri kwa matatizo yanayowasilishwa wanawake waliofanyiwa ukatili wa kijinsia, mashauri 461 yalipokelewa na kati ya hayo 63 yamepelekwa Mahakamani kwa ajili ya maamuzi zaidi.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudimu ya Bunge amesema kauli mbiu ya Siku ya Wanawake Duniani kitaifa kwa Mwaka 2026 ni Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050 inahimiza kujenga uelewa kwa jamii na wadau, kuwekeza kwenye Maendeleo Jumuishi ikiwemo kutambua Haki za Wanawake na Wasichana.
Amesema lengo lingine ni kuhakikisha Haki za Wanawake na Wasichana zinafanyiwa kazi kwa vitendo na kuleta mabadiliko ya kweli kama ilivyoainishwa kwenye nguzo za Dira 2050 .
Akizungumza katika Maadhimisho hayo Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kibaha Lea Lwanji amesema kwasasa wanaendelea kuratibu shughuli za wamachinga kwa kuwatambua na kuwasajili kwenye mfumo ambapo tayari wamachinga 1,112 kati yao wakes 732 wanaume 380.
Akielezea kuhusiana na uwezeshwaji kiuchumi Lwanji amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri imetenga sh. Biln 1.1 na kwamba mikopo yenye thamani ya sh.Billion 2.1 imetolewa kwa vikundi 436 na watu binafsi 21 kati ya vikundi hivyo 275 ni vya Wanawake ambao wamepata zaidi ya sh. Billion 1.
Ofisa Maendeleo huyo amebainisha kwamba Wajasiriamali wengi wamekuwa na mwamko wa kufanya biashara na wengi wanajitokeza kutafuta fursa za mitaji katika taasisi wezeshi.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa amewapongeza watumishi wanawake katika Manispaa hiyo kwa mchango wao katika ukusanyaji wa mapato uliowezesha Manispaa hiyo kushika nafasi ya pili kitaifa miongoni mwa Halmashauri 184 nchini Tanzania.
Dkt. Shemwelekwa amesema Manispaa ya Kibaha imefanikiwa kushika nafasi ya pili kitaifa katika ukusanyaji wa mapato baada ya kukusanya shilingi bilioni 17, huku idara ya Uhasibu na Mapato ikiongozwa na mwanamke.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo inaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ambapo kwa sasa imefikia shilingi bilioni 18, ikilinganishwa na awali ambapo ilikuwa ikikusanya shilingi bilioni 7.3.
No comments:
Post a Comment