Saturday, March 7, 2026

WANANCHI WAMIMINIKA KLINIKI YA ARDHI KIBAHA WAOMBA SIKU ZIONGEZWE

 

WANANCHI wa Manispaa ya Kibaha wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma katika Kliniki ya Ardhi ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki, huku baadhi yao wakiomba muda wa utoaji wa huduma hizo uongezwe kutokana na umuhimu wake.

Wananchi hao pia wameishukuru Serikali kwa kusogeza huduma hizo karibu yao na kueleza kuridhishwa na namna wanavyohudumiwa katika kliniki hiyo.

Maoni hayo yametolewa Machi 4, 2026, wakati kambi maalum ya kushughulikia masuala ya ardhi ikiendelea kwa siku ya tatu katika viwanja vya Maili Moja, Stendi ya Zamani, Manispaa ya Kibaha, ambapo wananchi wengi wameendelea kumiminika kupata huduma mbalimbali.

Mkazi wa Kibaha, Ester Joel, aliyefika katika kliniki hiyo kupata huduma ya hati, amesema ameridhishwa na huduma aliyoipata na kuomba muda wa kliniki hiyo uongezwe ili wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kuhudumiwa.

“Nimeridhika na huduma niliyoipata hapa. Kwanza nimepokelewa vizuri na nimeelekezwa namna ya kutatua changamoto yangu. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa huduma hii, ningependa siku ziongezwe hata kufikia wiki mbili,” amesema Ester Joel.

Kwa upande wake Coletha Nombo, ambaye pia alifika kupata huduma ya hati, amepongeza juhudi za Serikali kwa kuwaletea wananchi huduma hiyo karibu na maeneo yao.

Naye Ruth Kadema, mkazi wa Pangani, amesema ameridhishwa na huduma aliyoipata na kueleza kuwa amepewa maelekezo ya kufika tena siku ya Jumamosi kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kupata hati yake.

“Huduma hii ni nzuri sana. Nimeridhika na nimeambiwa nije Jumamosi kuchukua hati yangu baada ya kuwasilisha taarifa zangu leo,” amefafanua Ruth.

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa kambi hiyo maalum ya huduma za ardhi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi zinazohusu masuala ya ardhi, hususan umilikishwaji wa ardhi na upatikanaji wa hati.

Kambi hiyo maalum ya siku sita ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki ilianza rasmi Machi 2 na inatarajiwa kuhitimishwa Machi 7, 2026.

No comments:

Post a Comment