Sunday, March 29, 2026

KITUO CHA WANAWAKE WAJASIRIAMALI MANISPAA YA KIBAHA KUJENGA KIWANDA CHA KUTENGENEZEA BATIKI

NGUO za Batiki zimekifanya Kituo cha Wanawake Wajasiriamali Manispaa ya Kibaha kuitangaza Tanzania kwenye soko la Kimataifa ambapo ziliongoza kwa kununuliwa kwenye maonyesho nchi jirani. 

Akizungumza ofisini kwake Mjini Kibaha Mwenyekiti wa Kituo hicho Dk Magdalena Mangi alisema kuwa walishirki maonyesho kwenye nchi za Sudan, Kenya na Burundi miaka ya hivi karibuni ambapo zilinunuliwa kwa wingi.

Mangi alisema kufuatia batiki zao kuwa na soko kubwa wamejipanga kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa batiki ili kuongeza ubora wa bidhaa hiyo ili kuendelea kuitangaza nchi wanapokwenda kwenye maonyesho kama hayo siku za baadaye kwani wamedhamiria kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Mangi alisema kuwa kwa sasa wanazalisha batiki kwa kutumia mikono hali inayofanya ubora kupungua lakini wanaamini wakitumia mashine wataongeza ubora.

"Batiki tunazozalisha ni nzuri kwani tunatumia vitamba vizito ambavyo havichuji tofauti na wazalishaji wengine hali ambayo inatufanya tupate soko maeneo mbalimbali ambapo ushiriki kwenye nchi Burundi mwaka 2023, Sudan Kusini 2024, na Kenya 2025  tulipata mafanikio makubwa,"alisema Mangi.

Alisema kuwa wamekuwa wakipata masoko maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na watu binafsi na taasisi zikiwemo za watu binafsi na za serikali.

"Tuna soko japo siyo kubwa sana lakini tunataka tujitanue kwa kujitangaza kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii ili kuwafikia wateja wengi,"alisema Mangi.

Aidha alisema kuwa changamoto inayowakabili ni mtaji ambapo wakipata fedha watahakikisha wanajenga kiwanda ili kuongeza ubora wa batiki zao.

"Tulikopa Halmashauri kiasi cha shilingi milioni 40 ambapo bado tunaendelea na marejesho na tunahitaji sehemu ya kutengenezea batiki kwani hapa eneo ni dogo hali inayofanya tutengenezee nyumbani,"alisema Mangi.

Aliongeza kuwa wanaishukuru serikali kwa kuendelea kuwawezesha ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri na kuwawezesha hata kwa mikopo ya asilimia 10 ili kukuza biashara zao.

Naye Simon Kiondo mkufunzi wa masuala ya fedha na ujasiriamali alisema kuwa alikipatia elimu ya biashara mtandaoni ili kupata masoko zaidi kwani hiyo ni moja ya njia za kuongeza wateja.

Kiondo alisema kuwa baadhi ya changamoto ya vikundi vya ujasiriamali ni kukosa mipango na malengo na utunzaji wa kumbukumbu na ukosefu wa elimu ya fedha.

Alisema kuwa wajasiriamali wanapaswa kujitangaza na kwenda na wakati kwa kutumia teknolojia ya kisasa kupitia mitandao ya kijamii kuvutia masoko.

Kituo hicho kina jumla ya wanachama 10 na kinajohusisha na uzalishaji wa batiki, sabuni, mafuta mbalimbali, urembo, ushonaji nguo na khanga.

No comments:

Post a Comment