Thursday, March 5, 2026

MAOFISA USAFIRISHAJI WATAKIWA KUUNDA VIKUNDI WAKOPE HALMASHAURI





MAOFISA Usafirishaji maarufu kama Bodaboda kwenye Mtaa wa Mwendapole B wametakiwa kuunda vikundi ili waweze kukopa vyombo vya usafiri vinavyotolewa na Halmashauri kuachana na mikopo ya taasisi za watu binafsi ambazo zina gharama kubwa.

Aidha alisema kuwa gharama za mikopo ya Halmashauri ni ndogo na marejesho yake ni madogo tofauti na mikopo ya vyombo hivyo kwenye taasisi au watu binafsi.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo Abubakar Matumla wakati wa kikao na waendesha pikipiki wa Mtaa huo na kuwa wanashindwa kufanikiwa kwa kukopa pikipiki kwa riba kubwa.

Matumla alisema kuwa gharama za kukopa pikipiki kwa watu binafsi imekuwa ikiwafanya wasifanikiwe kutokana na gharama kuwa kubwa za mikopo hiyo hivyo hujikuta wanashindwa kujiongezea kipato.

"Serikali imewawekea mazingira mazuri ya mikopo yake kwani mnauwezo wa kukopa pikipiki, bajaji na Toyo kwa gharama nafuu na unarejesha kiasi kilekile ulichokopa na hakuna riba ya mkopo unaokopa hivyo ni wakati wenu wa kujiunga na kuwa na vikundi na mtumie fursa ya mikopo pale Halmashauri fedha zipo za kutosha na vyombo vya moto vipo,"alisema Matumla.

Alisema kuwa yuko tayari kuwasimamia kuhakikisha wanapata mikopo hiyo kwani hapendi kuona waendesha pikipiki wakitaabika ili hali kuna sehemu wanaweza kukopa bila ya kuwa na marejesho makubwa pia aliwataka kutoa taarifa kwa wale wanaojihusisha na vitendo vya kiuhalifu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha pikipiki hao Abdulatif Mbonganga alisema kuwa tayari wameshaanzisha kikundi kimoja na tayari kimeshasajiliwa kikiwa kinasubiri wakati ukifika waende kukopa.

Mboganga alisema kuwa changamoto kubwa kwao ni kukosa vyombo vya usafiri hali inayowabidi kukopa vyombo hivyo kwenye taasisi za watu binafsi ambazo zinagharama kubwa na kujikuta wakitumia nguvu kubwa kwenye marejesho.

Moja ya maofisa usafirishaji Salum Msaku alisema kuwa changamoto ya uhalifu inatokana na baadhi yao kuwapa ma "day worker" hasa nyakati za usiku ambapo wanawaletea sifa mbaya.

Msaku alisema kuwa ili kudhibiti hali hiyo kila mwendesha pikpiki aendeshe pikipiki yake na siyo kumpa mtu mwingine pia wahakikishe wanavaa riflector ambazo zitawatambua kwa namba zinazoandikwa mgongoni inakuwa rahisi katika ufuatiliaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Miembe Saba B Nuru Awadh alisema kuwa wanapaswa kuwa na ushirikiano na kuunda vikundi vya bodaboda ili wapate mikopo nafauu.

Awadh aliwataka wajiheshimu na wasijiunge na makundi mabaya kwani Rais amewapa kipaumbele vijana katika uongozi na sehemu mbalimbali ili wawe vinara kwa utendaji kazi.

No comments:

Post a Comment