MKOA wa Pwani umeanza maandalizi ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo kilele cha maadhimisho kimkoa yatafanyika Machi 8, 2026 katika Uwanja wa Ujamaa, Kata ya Umwe, Tarafa ya Ikwiriri, Halmashauri ya Mji Rufiji.
Mratibu wa maadhimisho hayo, Roseline Kimaro, amesema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge.
Akizungumza kuhusu maandalizi, Kimaro amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Dira 2050,” ikisisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia na haki kama nguzo ya maendeleo endelevu.
Amesema lengo ni kutambua na kuenzi mchango wa wanawake katika nyanja za kijamii, kisiasa na kiuchumi, sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Amebainisha kuwa kuanzia Machi 1 hadi 7 kutafanyika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma na kampeni za uhamasishaji kuhusu usawa wa kijinsia, kilele cha maadhimisho Machi 8.
Ameongeza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na kutoa wito kwa wananchi na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushiriki na kuunga mkono jitihada za kulinda na kuimarisha haki za wanawake na wasichana.

No comments:
Post a Comment