MTAA wa Machinjioni Kata ya Tangini umeishukuru Serikali kwa ujenzi wa kivuko kwenye barabara inayoelekea Shule ya Msingi Mamlaka kwa kuwaondolea adha ya wanafunzi kuvuka kwa kubebwa mgongoni.
Ujenzi wa kivuko hicho ambacho kimewekwa makalavati mawili kimeweza kuwaondolea adha wanafunzi wa shule hiyo ambapo kipindi cha mvua walishindwa kuvuka hadi wavushwe na watu wazima.
Akizungumza na Mwenyekiti wa Mtaa huo Aidan Mchiwa amesema kuwa mbali ya changamoto iliyokuwepo kwa wanafunzi lakini pia iliwakumba wakazi wa maeneo karibu na shule hiyo.
Mchiwa amesema kuwa manufaa ya kivuko hicho yameonekana ambapo mvua kubwa zilizonyesha juzi wanafunzi na wananchi wanavuka bila ya shida yoyote tofauti na ilivyokuwa awali ikiwa ni wakati wa siku 100 za Rais Dk Samia Suluhu Hassan.
"Eneo hilo ni mkondo wa maji hivyo mvua zinazonyesha maeneo mbalimbali maji yake yanapita hapo kwani ni eneo ambalo kuna bonde hivyo maji yanakuwa mengi na kusababisha adha kwa watu wanaopita kwenye barabara hiyo inayoelekea shuleni,"amesema Mchiwa.
Amesema kuwa serikali kupitia Halmashauri ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 9 na kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kujenga kivuko hicho ambapo hata magari na pikiiki yalikuwa yakipita kwa shida.
"Kuna maboresho kidogo yanatakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na mitaro na tukifanikiwa kupata fedha tutaichimba kwani bajeti tuliyopewa ya ujenzi wa kivuko hicho iliisha tutaomba kwa bajeti hii ili tuboreshe zaidi,"amesema Mchiwa.
Aidha amesema kuwa pia kwa kushirikiana na wananchi walifungua barabara tatu za Aidan, Nida na Kilima huku mbili zikiwa zimebakia za kwa Kapungu na kwa Landa.

No comments:
Post a Comment