Saturday, March 7, 2026

KIKUNDI CHA LULU YA WAJANE WAISHUKURU MANISPAA YA KIBAHA KWA MKOPO WA MILIONI 46

KIKUNDI cha wanawake cha Lulu ya Wajane kilichopo  Kongowe, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, kimeishukuru Manispaa ya Kibaha kwa kuwapatia mkopo wa shilingi milioni 46 uliowawezesha kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi, Mwenyekiti wa kikundi hicho Kanyenda Mweri amesema mkopo huo waliupata kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalum, na wamefanikiwa kuurejesha ndani ya kipindi cha miezi 11.

Amesema kikundi chao kinajishughulisha na ufugaji wa kuku wa aina mbalimbali, ambapo huuza kuku hao kwa jumla na rejareja na hivyo kuwa chanzo kikuu cha kipato kwa wanachama wake.

Aidha, amesema baada ya mafanikio waliyoyapata, kwa sasa wanatarajia kuomba mkopo mwingine ambao utawawezesha kununua mashine ya kutotolea vifaranga ili kupanua zaidi shughuli zao za ufugaji na kuongeza uzalishaji.

Kikundi hicho kimebainisha kuwa mkopo huo umewasaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao, sambamba na kutoa ajira kwa baadhi ya wananchi katika eneo lao.

No comments:

Post a Comment