Na John Gagarini, Kibaha
MAGARI ya kusafirisha abiria aina ya
Noah Hiace pamoja na pikipiki yamesababisha vifo vya watu 102 huku 246
wakijeruhiwa katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi Machi 2016.
Kutokana na kukithiri kwa ajali za
vyombo hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
(SUMATRA) mkoa wa Pwani imesitisha utoaji wa lesseni mpya kwa magari aina
ya Noah maarufu kwa jina la ‘Mchomoko’, na Hiace kwenye barabara
zote kuu ikiwamo barabara ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake mjini Kibaha ofisa mfawidhi wa SUMATRA mkoa wa Pwani Nashon Iroga alisema
kuwa kwa mujibu wa waraka walioupata kutoka makao makuu magari hayo
yote madogo ya abiria yanayokwenda masafa marefu kupitia
barabara kuu hayatapewa leseni ya kubeba abiria.
“Barabara kuu kuna vyombo vikubwa
vya usafiri hivyo hayataruhusiwa kupata leseni mpya badala yake
yaliyokwisha pata leseni yataendelea hadi hapo muongozo mwingine utakapo toka
tena,” alisema Iroga.
Alisema kuwa agizo hilo limetolewa
baada ya ongezeko kubwa la magari madogo ya kubeba abiria hasa magari aina
ya noah, kufanya safari ndefu huku baadhi yakiwa yamebeba abiria na
mizigo bila kuangalia usalama wa abiria na matokeo yake ni
kusababisha ajali za mara kwa mara na msongamano katika barabara kuu.
“Ukiangalia kwa hali ya kawaida magari
aina ya Noah yanabeba abiria wachache lakini ili wapate faida inabidi watoze
viwango vikubwa vya nauli, kubeba abiria kuliko uwezo wake na kwenda mwendo kasi ili
wafanye safari nyingi na kupata faida, matokeo yake wanahatarisha usalama
wa maisha ya abiria,” alisema Iroga.
Aidha alisema kuwa magari
hayo madogo yakiwamo Noah na Hiace yanayobeba abiria yatapewa lesseni mpya za
kufanya biashara kutumia ruti za barabara za ndani na sio barabara
kuu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment