Na John Gagarini, Kibaha
CHEMBA ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoa wa Pwani imemchagua Zainuddin Adamjee kuwa mwenyekiti wake ambaye ataongoza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Uchaguzi huo ulifanyika Mjini Kibaha mwishoni mwa wiki ambapo Adamjee ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kawe alichaguliwa bila ya kupingwa kutokana na kutokuwa na mpinzani ambapo uchaguzi huo uliitishwa baada ya uongozi uliopita kumaliza muda wake.
Viongozi wengine waliochaguliwa ni Ana Maridadi ambaye ni makamu mwenyekiti biashara, Karim Mtambo makamu mwenyekiti Kilimo na Mohamed Kiaratu mwakilishi wa mkutano mkuu Taifa.
Wengine waliochaguliwa ni Frank Mzoo mweka Hazina na Attiki Mohamed ambaye ni mjumbe wa kamati ambapo wagombea hao wote hawakuwa na wapinzani.
Akizungumza na wanachama na viongozi waliochaguliwa Rais wa TCCIA Taifa Injinia Peter Kisawilo alisema kuwa viongozi waliochaguliwa wanapaswa kuhakikisha wanawawekea mazingira mazuri wanachama ili waweze kuingia kwenye soko la ushindani la kimataifa.
Kisawilo alisema kuwa nchi ya Tanzania imeingia kwenye mikataba ya masoko makubwa yakiwemo yale ya Comesa, Sadc na la Afrika Mashariki ambapo wafanyabiashara wanapaswa kutengeneza bidhaa zitakazoingia kwenye ushindani na si kuwa watazamaji.
Kwa upande wake Adamjee alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha mkoa wa Pwani unakuwa moja ya mikoa ambayo inainua uchumi wake kutekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kuwa na viwanda ili nchi iwe na uchumi wa kati.
Adamjee alisema kuwa kwa kuwa mkoa huo una uzalishaji mkubwa wa bidhaa mbalimbali za kilimo, ufugaji viwandani na rasilimali za uvuvi hivyo una nafasi kubwa ya kuinua kipato cha wananchi wa mkoa.
Awali mwakilishi wa mgeni rasmi Anatoly Mhango ambaye alimwakilisha mkuu wa wilaya ya Kibaha alisema kuwa chemba hiyo ina nafasi kubwa ya kuwainua wanachama wake kupitia masoko ya ndani na nje.
Mhango alisema kuwa njia mojawapo wanayopaswa kuitumia ni kujitangaza ili watu waweze kujua fursa zinazopatikana kupitia chemba hiyo pia kupitia Chama Cha Kuweka na Kukopa SACCOS kilichopo ndani yake wanachama wanapaswa kurejesha mikopo kwa wakati ili watu wengi waweze kukopa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment